DIMBA PATRIOTS: Vipaji vya soka mtaani Kangemi
Na PATRICK KILAVUKA
DIMBA Patriots ilibuniwa mwaka huu kwa lengo la kuimarisha talanta na kuwapa wanasoka jukwaa la kuonesha uwezo wa vipaji vyao vya kandanda.
Hii ilikuwa baada ya wanasoka waliokuwa wakitandazia soka timu ya Dimba FC na mibabe wa Kangemi Patriots kuletwa pamoja kujenga timu nzito ya kusukuma gurudumu la kabumbu katika ligi ya FKF Tawi la Nairobi Magharibi.
Inafanyia mazoezi Shule ya St Michael barabara ya Jogoo japo inachezea michuano ya ligi ya Shirikisho la Soka Kenya uwanjani Kabete Vetlab.
Kulingana na meneja wa timu Naftali Aseka ambaye amewahi kuichezea klabu ya Dimba, anasema azimio la kustawisha timu hii limeafikiwa kwa sababu kuna wachezaji ambao wanaonesha ujuzi wa kusakata boli kwa weledi na kuipelekea timu hii kunawiri sana katika muda mfupi imestawishwa.
Inaoongezwa na kocha Mustafa Mohammed (alizichezea timu mahiri kama Sofapaka, Nakumatt, AFC Leopards, Chemelil na Harambee Stars kama fowadi), kinara Dickson Arudo na meneja Aseka.
Imefanya kweli katika ligi hiyo licha ya kwamba ni timu ya kujitegemea. Imemaliza ya nne bora baada ya kushuka dimbani mara 30 na kuzoa alama 54.
“Haijakuwa rahisi kufikia ufanisi huu kwa sababu ni mara yetu ya kwanza kushiriki ligi hiyo japo tunajifadhili. Kuchota alama hizo ni jambo la kujivunia. Tunalenga kumaliza katika mduara wa tano bora msimu huu na ndoto yetu imetimia na tunashukuru Mola kwa kutuwezesha,” alieleza meneja Aseka na kuongezea kwamba, wapo na matumaini ya hata kuvuka Daraja ya Pili ya Ligi ya Taifa watakapomaliza ligi msimu ujayo.
Matumaini waliokuwa nayo ndiyo yaliwatia changamoto ya kujikasa kiume kuhakikisha wamepata ushindi ukiwemo wa michuano wa mwisho na ligi.
Katika mechi za kuelekea mwisho wa mkumbo, timu hii ilipata ushindi dhidi ya Gogo Boys baada ya kuilima 2-1 uwanjani Kihumbuini, kuirambisha sakafu South B Sportiff 2-0 uga wa Magereza Langata, kuipachika AFC Leopards 2-1 uwanjani Kabete Vetlab, kunyolewa na Riruta Makarios III kwa ushindi mwembamba wa 2-1 uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kinyanjui.
Hatimaye, ilitoa kijasho Slum Dwellers kwa kuizaba 1-0 na kukwangura Kitisuru All Stars 2-1.
Imetoa wachezaji kama difenda Gregory Nyapala ambaye alijiunga na kambi la Kangemi All Stars, beki George Abuya aliyesajiliwa na zizi la MOYAS, Benard Karanja aliyenaswa Savanna FC na Amos Ogoda ambaye anapigia soka Migori Youth.
Kikosi cha timu kinajumuisha Peter Mwangi, Robert Nyaga, Samuel Mwangi, Michael Ochola, Martin Sila, Richard Wambua, Justice Muchiri, Kevin Masau, Julius Maluki, Abudullahi Kithome, Abubakar Abudi na Shakur Huka.
Wengine ni Gideon Musyoki, Joash Birongo, Ahmed Nasir na Nicholas Olum.