Telkom yatangaza kutimua wafanyakazi 500
Na PETER MBURU
KAMPUNI ya Telkom Ijumaa imetangaza kuwa itawapiga kalamu wafanyakazi wake 500, katika mpango wake wa kupunguza gharama ya matumizi.
Kupitia ujumbe iliotuma kwa vyombo vya habari, kampuni hiyo ilitoa ilani ya siku 30 kwa Wizara ya Leba, kumaanisha kuwa wafanyakazi hao wataondolewa kazini Novemba.
Hii ni baada ya kampuni hiyo kupinga kuwa ilikuwa ikipanga kuwafuta kazi wafanyakazi wake wiki mbili zilizopita, ambapo ilijitetea kuwa ilikuwa ikilenga kuinua utendakazi na kupanua soko.
Kampuni hiyo inasemekana kuipa kazi kampuni ya Mckinsey kuifanyia ukaguzi, ambayo ilipendekeza idadi hiyo ya wafanyakazi wachujwe.
“Mahusiano yetu na Mckinsey ni kwa ajili ya kuinua utendakazi wa kampuni na kupanua soko. Hakuna mpango wa kuwafuta kazi wafanyakazi,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Telkom Aldo Mareuse.
Lakini katika ujumbe wake wa Ijumaa, kampuni hiyo ilijitetea kuwa kuwaondoa wafanyakazi hao kunanuia kuipandisha hadi kuwa nambari mbili kati ya kampuni zinazotoa huduma za simu.
“Kwa hivyo inatuhitaji kufanya mabadiliko kwenye biashara yetu na hivyo hii itakuwa na adhari za muda mfupi na mrefu kwa wafanyakazi,” ujumbe huo ukasema.
Kwa sasa, kampuni hiyo ina takriban wateja milioni nne, ikilinganishwa na washindani wake Safaricom inayoongoza kwa wateja 29.7milioni na Airtel iliyo na wateja zaidi ya milioni tisa.
Kampuni hiyo inamilikiwa kwa ushirikiano wa Serikali iliyo na asilimia 40 ya hisa na kampuni ya Helios Investment Partners yenye hisa asilimia 60.