• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:44 AM
Wanafunzi wengi huhitimu Kidato cha Nne bila kujua kusoma wala kuandika – Ripoti

Wanafunzi wengi huhitimu Kidato cha Nne bila kujua kusoma wala kuandika – Ripoti

Na VALENTINE OBARA

WANAFUNZI takriban 200,000 wanaokamilisha Kidato cha Nne nchini kila mwaka huwa hawajui kusoma na kuandika, ripoti imeonyesha.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 40 ya watu wenye umri wa kati ya miaka 19 na 20 waliohitimu kutoka shule za upili humu nchini wana udhaifu mkubwa wa kusoma na kuandika.

Idadi hiyo inaweza kukadiriwa kuwa jumla ya wanafunzi 240,000 kila mwaka ikizingatiwa kuwa kwa miaka ya hivi majuzi watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) wamekuwa 600,000 kwa wastani.

“Hili ni tatizo kubwa ikizingatiwa kuwa uwezo wa kusoma na kuandika ni hitaji muhimu la mtu kufanikiwa katika mazingara ya kikazi,” inasema ripoti hiyo kuhusu mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa katika utendakazi ulimwenguni.

Lawama ilielekezwa kwa jinsi serikali na wanasiasa wanavyotumia rasilimali nyingi kwa ujenzi wa miundomisingi ya elimu bila kujali kuhusu mahitaji mengine muhimu kama vile idadi ya walimu wa kutosha na mafunzo yanayotolewa kwa walimu hao kabla waruhusiwe kuingia darasani.

“Serikali nyingi hupenda kutumia fedha zaidi kwa vitu vinavyoweza kuonekana kama vile ujenzi wa shule na hospitali, huku kiwango kidogo mno kikiwekezwa kwa ubora na uwezo wa kitaalamu kwa walimu na maafisa wa afya,” ikasema.

Ripoti hiyo iliongeza: “Wanasiasa wanapofanya kampeni mara nyingi huwa wanaahidi shule mpya na hospitali lakini ni nadra kwao kujadili kuhusu hali halisi ya elimu.”

Kulingana na Benki ya Dunia, hii ni kutokana na kuwa wanasiasa hutaka njia ambayo inaweza kuwaletea sifa kwa haraka ilhali uwekezaji katika ubora wa elimu badala ya miundomsingi huchukua muda mrefu kabla matokeo yake yaonekane.

Kwa miaka mingi, ujenzi wa madarasa na uboreshaji wa miundomsingi ya shule umekuwa ukipewa kipaumbele na wabunge kupitia kwa Hazina ya Kustawisha Maendeleo katika Maeneobunge (CDF).

Kwa upande mwingine, Serikali za Kaunti zimekuwa zikiwekeza pakubwa katika ujenzi wa shule za chekechea ambazo usimamizi wao ulikabidhiwa kwao kikatiba.

Utafiti uliofanywa na shirika hilo katika mtaa wa mabanda jijini Nairobi ulibainisha kwamba ingawa idadi ya watoto waliojiunga na shule za chekechea imeongezeka, mafunzo wanayopewa hayana maana kwa watoto wa umri wao ambao ni wa miaka kati ya mitatu na sita.

Ilibainika kwamba watoto wa chekechea hufunzwa kwa msingi wa mtaala unaowahitaji kufanya mitihani mwishoni mwa muhula ilhali watoto wa umri huo hustahili tu kupewa ujuzi wa kimsingi kuendeleza masomo yao baadaye.

“Elimu duni ya chekechea husababisha matokeo mabaya badala ya kuwapa uwezo wa watoto kuboresha lugha, kutambua mambo na kushirikiana na wenzao katika jamii,” ikasema ripoti.

You can share this post!

Obado sasa alazimika kuhama nyumbani

Wanafunzi wengi huabudu shetani nchini – Maaskofu

adminleo