Makala

KPA, Mkuu wa Sheria wapinga kaunti isimamie bandari ya Mombasa

October 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PHILIP MUYANGA

Halmashauri ya Bandari nchini (KPA) na mkuu wa sheria wamepinga kesi iliyowasilishwa mahakamani na wakazi wa Mombasa wakitaka jukumu la kusimamia bandari litwikwe serikali ya kaunti ya Mombasa.

Wanataka kesi hiyo kutupiliwa mbali wakisema kuwa haikuwa na msingi wowote na chanzo chake kilikuwa ni kutoelewa sheria.

KPA, kupitia aliyekuwa mkuu wa sheria Prof Githu Muigai, Bw Nani Mungai na Geofrey Imende walisema kuwa kesi hiyo inaenda kinyume na mikakati ya kusuluhisha mizozo ilivyowekwa na katiba.

“Kesi hii inazua swala ambalo limeshatatuliwa kabisa na mahakama ya rufaa,”alisema Prof Muigai.

Jopo la majaji watano ndilo linalosikiza kesi hiyo,wao ni Jaji Lydia Achode, Eric Ogola, Anthony Mrima, Joel Ngugi na Pauline Nyamweya.

Wakili mwingine wa KPA Bw Mungai alisema kuwa kulikuwa na kesi nyingine sawia na ambayo iliyoko mahakamani inayojadili maswala kama hayo ndiposa jopo la majaji lisikubali kesi kuendelea kuzuia mahakama tofauti kutoa maamuzi ambayo hayafanani.

Kupitia wakili wa serikali Nguyo Wachira,mkuu wa sheria alisema kuwa mizozo baina ya ngazi mbili za serikali lazima itatuliwe kwa majadiliano.

Bw Wachira alisema kuwa kesi ya wakaazi hao wa Mombasa inafaa kutupiliwa mbali na sheria kuhusu utatuaji wa mizozo baina ya ngazi mbili za serikali kuendelezwa.

Bw William Ramogi, Bi Asha Omar na Bw Gerald Kiti, ambao ni waweka kesi kupitia wakili wao Caroline Oduor walipinga ombi la mkuu wa sheria na KPA la kutaka kesi yao kutupiliwa mbali.

Bi Oduor alisema kuwa msingi wa kesi yao ni ukiukaji wa haki za kikatiba.

Aliomba mahakama kutupilia mbali ombi la KPA na mkuu wa sheria na kusikiza na kuamua kesi walioiwasilisha.

Serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia wakili Pheroze Nowrojee ilisema kuwa maombi ya waweka kesi hayawezi kupeanwa na sheria kuhusu mizozo baina ya ngazi tofauti za serikali.

Bw Nowrojee alisema kuwa mahakama ilikuwa mahali bora kwa kuangazia maswala yaliyowasilishwa na wakazi wa Mombasa ambao malalamishi hayahusishi maamuzi ya kisiasa au serikali kuu.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu (Muhuri) na mwaharakati Maina Kiai walisema kuwa wakati haki za watu zinatishiwa, mahali pa kupata usaidizi ni mahakama kuu.

Bw William Ramogi, Bi Asha Omar na Bw Gerald Kiti wanasema katika kesi hiyo ya kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa,kikatiba imepewa mamlaka ya kusimamia maswala ya uchukuzi wa kaunti.

Wameswashtaki mkuu wa sheria,waziri wa uchukuzi,halamashauri ya bandari nchni (KPA) na shirika la reli nchini.

“Ni kinyume cha katiba kwa serikali ya kitaifa kutofanya ugatuzi shughuli za usimamizi wa bandari katika serikali ya kaunti,”watatu hao wanasema katika kesi yao.

Wanasema kuwa bandari kuu katika maeneo tofauti ulimwenguni zilijengwa na serikali zao lakini zinasimamiwa na miji ambayo iko.

Mahakama kuu itatoa uamuzi wake Ijumaa.