• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
OBARA: Msako umeonyesha jinsi abiria huhatarisha maisha

OBARA: Msako umeonyesha jinsi abiria huhatarisha maisha

Na VALENTINE OBARA

UHABA wa magari ya uchukuzi wa umma ulioshuhudiwa Nairobi wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii, umeibua maswali kuhusu usalama wa magari ambayo wananchi wamekuwa wakitegemea kwa safari zao mjini.

Huku msako kamili wa magari yasiyostahili kuwa barabarani ukipangiwa kuanza leo, jambo la muhimu zaidi linalopaswa kuzingatiwa na wadau wote ni usalama wa abiria na watumizi wengine wote wa barabara zetu.

Jumatatu iliyopita, wamiliki wengi wa magari ya uchukuzi wa umma waliamua kutoyapeleka barabarani baada ya polisi wa trafiki kukamata kadhaa yaliyopatikana hayastahili kuhudumu barabarani siku ya Jumapili. Wamiliki hawa walihofia magari yao yangezuiliwa na watozwe faini.

Hali hii ilikuwa inaashiria kwamba magari yao hayakuwa yanahudumu yakiwa yametimiza matakwa ya kisheria kuhusu usalama barabarani.

Inapaswa tukumbuke kuwa ukiukaji wa sheria za barabarani huwa haudhuru tu wale walio ndani ya gari lisilofaa kuwa barabarani, bali ajali ikitokea inaweza kudhuru pia waendeshaji magari ambao wamefuata sheria kikamilifu, mbali na wapita njia wasio na hatia yoyote.

Si siri kwamba ufisadi uliokithiri katika sekta ya uchukuzi wa umma ndio hufanya baadhi ya wamiliki wasiogope kuvunja sheria kwani wanajua kwamba kuna njia rahisi ya kuepuka kuadhibiwa.

Utasikia baadhi yao wakisema ni heri watoe hongo kuliko kulazimika kufuata mkondo wa adhabu za kisheria kwani wanaona watapoteza muda mwingi wakipelekwa kortini.

Ufisadi

Wakati mwingi suala kuhusu ufisadi barabarani linapojadiliwa, utakuta kwamba wahudumu wa magari ya umma na wakuu wa maafisa wa polisi hulaumiana kuhusu upande ambao hufanya tatizo hili kukithiri.

Kwa upande mmoja, utasikia wamiliki na wahudumu wa magari wakidai wasipokubali kutoa hongo, hata kama wamefuata sheria, polisi watawahangaisha na kuwaharibia biashara yao.

Kwa upande mwingine, wakuu wa polisi nao hudai kuwa kusingekuwa na ulaji rushwa iwapo wahudumu wa magari hayo wangekataa kutoa hongo.

Kinachohitajika ni pande hizi mbili zikubali kuwa kuna ufisadi ambao unasababisha maafa yanayovuruga familia nyingi mara kwa mara na tabia hii ikomeshwe mara moja.

Uhai wa binadamu hauwezi kulinganishwa na vito vya thamani yoyote humu duniani, na huwa ninashangaa sana ninapowaza jinsi afisa wa polisi anaweza kuendeleza maisha yake kwa starehe akijua zile Sh50 alizopokea kama mlungula zilisababisha vifo vya watu 50 ajalini. Yani uhai wa binadamu uliuzwa kwa Sh50 pekee!

Mbali na haya, idara ya mahakama pia inastahili kuweka mikakati itakayohakikisha kwamba kesi kuhusu ukiukaji wa sheria barabarani zinatatuliwa kwa kasi na kwa njia ya uwazi bila kudhulumu haki za wahudumu wa magari.

Hofu ya kutotendewa haki kortini ni sababu nyingine ambayo hufanya wananchi kutafuta njia haramu za mkato kama vile utoaji rushwa na matokeo yake ni kukuzwa kwa ukiukaji wa sheria unaozaa madhara mengi kwa jamii.

You can share this post!

TAVETA: Wagonjwa wa saratani kupata afueni katika kituo...

TAHARIRI: Serikali isiwatie hofu watahiniwa

adminleo