Michezo

Afrika Kusini yaahidi mabinti wa kikosi cha soka mamilioni wakishinda AWCON

November 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka la Afrika Kusini (SAFA) litamtuza kila kipusa marupurupu ya Sh1,141,397 kwenye timu ya Banyana Banyana ikishinda Kombe la Afrika la wanawake (AWCON) litakaloandaliwa nchini Ghana kutoka Novemba 17 hadi Desemba 1, 2018.

Zawadi hii ni kando ya Sh285,281, ambayo kila mchezaji anapokea kwa kushiriki kombe hilo la mataifa manane.

Banyana Banyana imeahidiwa Sh820,179 kwa kila mchezaji ikimaliza kombe hilo na medali ya fedha na Sh713,732 kila mmoja ikishinda medali ya shaba.

Timu zitakazoshiriki makala ya mwaka huu ni Ghana (wenyeji), Nigeria (mabingwa watetezi), Cameroon, Afrika Kusini, Algeria, Mali, Zambia na Equatorial Guinea, ambayo ilipokonywa tiketi na kupewa Kenya kabla ya kurudishiwa tena.

Kenya imekataa rufaa kuhusu uamuzi wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuipokonya tiketi ikisisitiza Equatorial Guinea ilichezesha mchezaji asiye halali dhidi yake wakati wa mechi za kufuzu kushiriki dimba hili.

Equatorial Guinea pia inatumikia marufuku kutoka kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa visa vingi vya kutumia wachezaji ambao si wa taifa hilo.