• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Viongozi wa Kiambu wataka Ngilu akamatwe

Viongozi wa Kiambu wataka Ngilu akamatwe

GAVANA wa Kitui Bi Charity Ngilu akihutubu. Picha/ Maktaba

Na KITAVI MUTUA na ERIC WAINAINA

Kwa Muhtasari:

  • Bi Ngilu asema lori lililochomwa lilikuwa limezuiliwa na polisi na hivyo basi polisi ndio wanafaa kueleza yaliyotokea
  • Apuuzilia mbali video inayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inadaiwa ilinaswa akipochochea wakazi
  • Viongozi wa Kitui na Makueni wamtetea Ngilu kuhusu uamuzi wake wa kupiga marufuku biashara ya makaa

VIONGOZI wa Kaunti ya Kiambu wametaka Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu, akamatwe mara moja kwa madai kuwa alichochea wakazi kuchoma magari yanayopatikana yakisafirisha makaa kutoka kaunti yake.

Hata hivyo, Bi Ngilu Jumapili alikana madai hayo akisema lori lililochomwa wiki iliyopita lilikuwa limezuiliwa na polisi na hivyo basi polisi ndio wanafaa kueleza yaliyotokea.

Mbunge wa Limuru, Bw Peter Mwathi, alimtaka Inspekta Jenerali wa polisi, Bw Joseph Boinnet, ahakikishe Bi Ngilu amekamatwa na kushtakiwa kuhusiana na kisa hicho ambapo lori la mfanyabiashara wa Limuru lilichomwa na wakazi wa Kitui.

Alipohutubia waandamanaji waliokasirishwa na uchomaji huo wa lori na ambao waliziba barabara ya Nairobi-Nakuru Jumamosi wakiandamana, Bw Mwathi alidai kuwa matamshi ya gavana huyo ndiyo yalisababisha kisa hicho.

“Kama una mashabiki, kwa wale wanaoelewa soka, na mashabiki wawe watovu wa nidhamu, klabu hutozwa faini. Katika kisa hiki, gavana mwenyewe ndiye alisimamisha gari hilo na ni lazima anafahamu wahusika waliolichoma,” akasema.

 

Haieleweki

Lakini alipozungumza katika mazishi ya Bw Michael Musambi, ambaye alikuwa mfanyakazi katika serikali ya kaunti ya Kitui, Bi Ngilu alisema lori hilo lilikuwa limezuiliwa na polisi katika eneo la Kanyonyoo na haieleweki kwa nini polisi walishindwa kuzuia lisichomwe.

Alipuuzilia mbali video inayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inadaiwa ilinaswa alipochochea wakazi, akisema video hiyo imenuiwa kupotosha wakazi dhidi ya kutetea uhifadhi wa mazingira yao na kuwaharibia viongozi sifa.

“Nina jukumu la kuchukua hatua mwafaka kulinda mazingira yetu ili kukabiliana na ukame wa mara kwa mara na uhaba wa mvua katika eneo hili,” akasema.

Viongozi wa kaunti za Kitui na Makueni walimtetea Ngilu kuhusu uamuzi wake wa kupiga marufuku biashara ya uchomaji makaa katika kaunti yake.

You can share this post!

Uhaba mkubwa wa damu wakumba Kenya

Marehemu arejeshwa mochari kwa kukosa pa kuzikwa

adminleo