• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Msinisukume kumtambua Uhuru kama Rais wa Kenya, Raila awaambia mabalozi

Msinisukume kumtambua Uhuru kama Rais wa Kenya, Raila awaambia mabalozi

Kinara wa muungano wa NASA na mwenyekiti wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA na WANDERI KAMAU

Kwa Muhtasari:

  • Bw Odinga asema mabalozi wamekuwa wakipendelea Serikali ya Jubilee na hivyo hawezi kuwasikiza
  • Mabalozi walitaka upinzani ukubali  kwamba uchaguzi wa marudio wa urais Oktoba 26, 2017 ulifuata sheria
  • Bw Odinga amesisitiza kuwa alishinda uchaguzi wa Agosti 8, 2017 licha ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi huo

KIONGOZI wa Muungano wa NASA, Raila Odinga, Jumapili aliwafokea mabalozi wa mataifa ya magharibi kwa kumsukuma atambue uhalali wa Rais Uhuru Kenyatta kama kiongozi wa taifa aliyechaguliwa kikatiba.

Bw Odinga alisema mabalozi hao wamekuwa wakipendelea Serikali ya Jubilee na hivyo hawezi kuwasikiza.

Kiongozi huyo alikuwa akijibu mwito wa mabalozi wa mataifa 11 ambao wamemtaka yeye pamoja na viongozi wenzake wa NASA kumtambua Rais Kenyatta katika kile walichosema ni hatua ya kwanza katika kuanzisha mazungumzo ya kitaifa.

 

‘Hatuhitaji ushauri wa mabalozi’

“Hamuwezi kuamulia Wakenya rais wao ni nani. Kenya ni nchi huru na shida za Wakenya zitatatuliwa na Wakenya wenyewe. Wakenya waliona mienendo yao walipokuwa waangalizi wa uchaguzi Agosti 8. Hatuhitaji ushauri kutoka kwa balozi wa Amerika wala wa Uingereza,” akasema.

Alikuwa akihutubia umati baada ya kutembelea waathiriwa wa mkasa wa moto uliotokea mwishoni mwa Januari katika mtaa wa Kijiji, eneobunge la Langata, kaunti ya Nairobi.

Taarifa iliyotolewa na mabalozi, miongoni mwao Robert Godec wa Amerika, Nic Hailey (Uingereza) na Juta Frasch (Ujerumani) mnamo Jumamosi ilitaka viongozi wa upinzani wakubali uamuzi wa Mahakama ya Juu kwamba uchaguzi wa marudio wa urais Oktoba 26, ulifuata kanuni za kisheria.

 

Kukubali matokeo

“Uhuru Kenyatta na William Ruto ndio Rais na Naibu Rais halali wa Jamhuri ya Kenya. Viongozi wa upinzani wanafaa kukubali hili kabla ya kuwa na mashauriano ambayo wanataka pamoja na Wakenya wengine wengi,” ikasema taarifa hiyo.

Mabalozi wengine waliotia sahihi taarifa hiyo ni Alison Chatres (Australia), Sara Hradecky (Canada), Mette Knudsen (Denmark), Anna Jardfelt (Sweden), Victor Conrad Ronneberg (Norway), Frans Makken (Uholanzi), Tarja Fernandes (Finland) na Kim Ramoneda (Ufaransa).

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa alishinda uchaguzi wa Agosti 8, 2017 licha ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi huo na kuagiza mwingine ufanyike Oktoba 26, ambao NASA walisusia. Wabunge wa mrengo wa NASA na viongozi wengine pia wamesema hawatambui Serikali ya Rais Kenyatta.

 

Onyo

Kwenye taarifa yao, mabalozi walionya kuwa misimamo mikali kati ya Serikali na NASA kuhusu masuala tata ya kisiasa inahatarisha uthabiti wa demokrasia nchini.

“Ni lazima pande husika zitathmini kwa kina mustakabali wa kidemokrasia nchini zinapoendelea kushikilia misimamo mikali kuhusu utata unaotokana na chaguzi mbili za 2017,” wakasema.

Mabalozi wamekuwa miongoni mwa wadau ambao wanajaribu kupatanisha Jubilee na NASA lakini juhudi zao hazijafaulu.
Katika ziara yake jana, Bw Odinga alipuuzilia mbali ajenda nne kuu za Jubilee kuhusu maendeleo na kusema mipango hiyo haitafaulu kutokana na kile alisema ni ufisadi serikalini.

 

Domo kaya

“Hayo yote ni domo kaya. Maneno matupu ambayo hayana maana. Hakuna maendeleo ambayo Jubilee italetea taifa letu hata wakikaa miaka mia moja,” akasema.

Viongozi waliohutubu katika mkutano huo walidai mtaa wa Kijiji ulichomwa na matapeli wanaolenga kufurusha wakazi ili wanyakue ardhi hiyo.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na Mbunge wa Ruaraka Tom Kajwang’ na Mbunge wa Dagoretti Kusini Simba Arati miongoni mwa wengine.

Bw Kajwang’ ambaye sasa amejibandika jina la ‘Jaji Mkuu katika Jamhuri ya Wananchi’ alitoa wito kwa kiongozi huyo wa Chama cha ODM aunde ‘serikali kamili’ ikiwemo kubuni baraza la mawaziri na kuajiri mabalozi.

You can share this post!

Marehemu arejeshwa mochari kwa kukosa pa kuzikwa

Miguna Miguna: Nilivyokula samaki ‘kwa macho’...

adminleo