• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
AFCON2019: Limbukeni wawili kuramba urojo wa soka ya bara

AFCON2019: Limbukeni wawili kuramba urojo wa soka ya bara

NA CECIL ODONGO

MECHI za kuwania taifa bingwa Barani Afrika (AFCON) mwaka 2019 zitashirikisha timu mbili geni ambazo hazijawahi kuonja au kushiriki fainali hiyo tangu izinduliwe miaka ya nyuma.

Mataifa ya Madagascar na Mauritania yamefuzu kushiriki makala ya  fainali ya mwaka 2019 na yatajiunga na mengine 10 ambayo tayari yamejihakikishia nafasi ya kutua nchini Cameroon mwakani kwa ajili ya kidumbwedumbe hicho.

Mauritania watashiriki AFCON kwa mara ya kwanza baada ya kufuzu walipotoka nyuma na kuishinda Botswana  2-1 nyumbani huku mshambulizi wao matata Ismael Diakite akiwafungia bao la kihistoria la ushindi katika dakika ya 84 lililowapa ushindi.

Mabingwa wa AFCON mwaka wa 2012 Zambia hata hivyo watakosa Makala ya AFCON  kwa mara ya pili  baada ya kukosa Makala ya mwaka wa 2017. Maarufu kama ‘The Chipolopolos’ Zambia ilikung’utwa 1-0 na wanyonge Mozambique, matokeo ambayo  yalitamatisha azma yao ya kuelekea Cameroon huku kushindwa huko  kukizidi kuombolezwa na raia wa taifa hilo wanalohusudu mchezo wa soka kama mboni ya jicho.

Mshambulizi wa Manchester City Riyad Mahrez naye alihamisha uweledi wake akisakatia mabingwa hao wa ligi ya Uingereza hadi timu ya taifa ya Morocco pale alipong’aa mchezoni na pia kuifungia nchi yake mabao mawili yaliyoisaidia kuinyuka Togo 4-0 nyumbani.

Kenya na Ghana pia wako pua na mdomo kufuzu japo bado zinasubiri mawasiliano rasmi kutoka kwa Shirikisho la soka barani Afrika(CAF) kushadidia uamuzi wa kuipiga marufuku Sierra Leone ambayo haijashiriki mechi tatu za kiny’ang’anyiro hicho.

Jumla ya mataifa 14 yamejikatia tiketi:  Senegal na Madagascar (Kundi A), Morocco na Cameroon (Kundi B), Mali (Kundi C), Algeria (Kundi D), Nigeria (Kundi E), Guinea na Ivory Coast (Kundi H), Mauritania (Kundi I), Tunisia na Misri (Kundi J) na Uganda (Kundi L).

  • Tags

You can share this post!

#AFCON2019: Mataifa 14 yafuzu

SHAIRI: Ukapera siachi, muhibu sipati

adminleo