KAULI YA WALIBORA: Usiivyoge lugha kimatumizi iwapo huimanyi barabara
NA PROF KEN WALIBORA
Ninapenda kusikiliza idhaa ya Kiingereza ya BBC sio tu kwa sababu ya kuarifiwa, kuburudishwa, na kufundishwa bali pia kwa sababu ya lugha nzuri ya watangazaji wake.
Watangazaji hao aghalabu husarifu lugha kwa heba na mvuto wa aina yake. Mpenzi wa lugha hapa nilipo, siwezi kukichukia Kiingereza kwa sababu ya kukipenda Kiswahili.
Lakini mapema wiki hii nimechukia Kiingereza cha BBC. Alitokea ripota mmoja akawa anaripoti kuhusu masaibu ya mazeruzeru katika Kisiwa cha Ukerewe. BBC walimbebesha mzigo mkubwa wa kuwasilisha ripoti yake kwa Kiingereza.
Katika dakika mbili au tatu alizowasilisha ripoti yake, hakuna hata sentensi moja ya Kiingereza iliyokuwa sahihi. Mwanahabari huyu maskini kalazimika kuaibisha Afrika Mashariki duniani kwa Kiingereza cha ajabu ajabu. Mara “They come from different part of the country” mara “The government operate in this area,” n.k.
Mimi nasema kama lugha huiwezi achana nayo. Mimi leo ukiniambia nizungumze Kifaransa siwezi, maana sikijui mbele wala nyuma yake. Ndivyo ilivyo ukiniambia nizungumze Kikerewe, Kikamba, Kihausa, Kichina au Kirusi. Kiingereza naweza kidogo, kwa hiyo nitajitahidi niseme mawili matatu.
Sidhamirii kujitanua kifua, lakini Kiingereza nilichokisikia kutoka kwa yule ripota kilinishtua. Nilijiuliza maswali mengi sana. Mwanzo, je ilikuwa lazima awasilishe ripoti yake kwa Kiingereza? Amelazimishwa au amejilazimisha?
Hilo lanikumbusha mdahalo wa tangu jadi wa lugha ya uandishi kwa waandishi wa Kiafrika. Ni vigezo gani anavyopaswa kuvitumia mwandishi kuchagua lugha ya maandishi yake? Mhakiki wa Kinaijeria, Obi Wali alisema kwamba fasihi ya Kiafrika ilikuwa haina mustakabali kwa vile waandishi wengi wamekimbilia kuandika lugha za kigeni.
Alidai fasihi ya Kiafrika inaelekea kudumaa kutokana na uteuzi mbaya wa lugha.
Ingawa waandishi kama vile Chinua Achebe waliibuka na kutetea matumizi yao ya Kiingereza kubeba tajiriba yao ya Kiafrika, suala la uteuzi wa lugha bado halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Ukweli ni kwamba waandishi wa Kiafrika wanaoandika kwa kutumia lugha asilia kama vile Kiswahili, Kiigbo, Kisomali na Kizulu, hawajulikani nje ya mipaka ya lugha zao na vijiji vyao.
Kuhusu Kiswahili hata wapo wanaodai si lugha ya Kiafrika bali inayotokana na Kiarabu. Watu wameandika hata vitabu na kuwafundishia mamilioni ya wanafunzi katika mifumo ya elimu kwamba ndivyo ilivyo asili ya Kiswahili. Kiswahili kimekoseshwa Uswahili na Uafrika wake na kuarabishwa.
Ushauri wangu kwa waandishi chipukizi siku zote huwa ni kwamba ni heri kuandika katika lugha inayokutirikia kwa mazoea.
Lugha ambayo ukiyaita maneno yanaitika kwa urahisi. Kwa baadhi ya waandishi lugha hiyo inaweza kuwa ni lugha yao asilia au lugha ya mawasiliano mapana kule wanakotokea.
Ilimuradi lugha anayoichagua mwandishi inakuwa chombo cha kuwasilishia ujumbe wa sanaa yake, si hoja kama yeye ni mzawa au si mzawa wa lugha hiyo. Tatizo linazuka wakati anakosa ujuzi wa kukitumia chombo hiki kama mwanahabari aliyetuborongea Kiingereza.