• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
DHULUMA: Niliosha maiti kwa siku 40 bastola ikiwa kichwani, asimulia mjakazi wa Huruma

DHULUMA: Niliosha maiti kwa siku 40 bastola ikiwa kichwani, asimulia mjakazi wa Huruma

NA CECIL ODONGO

MASKINI hana lake, tena maskini kupata haki ni tajiri kupenda na kuipata haki yenyewe ni kibarua kigumu kama kuukwea mchongoma.

Ndiyo hali aliyokumbana nayo Penninah Owuor mwaka wa 2017 baada ya mwaajiri wake Mohammed Abdi Noor kumlazimisha kumwosha maiti akiwa ameelekezewa mtutu wa bunduki kichwani kwa siku 40.

Bi Owuor ambaye ni yatima anatoka Magharibi mwa nchi na umaskini mkubwa wa familia yake ulichangia yeye kupata kazi kama mjakazi katika nyumba ya Bw Noor mtaani Huruma jijini Nairobi baada ya jamii yake iliyosalia kumwoonyesha ukatili mkubwa akiishi nao mashinani.

Hata hivyo alielezwa na mkewe Bi Noor alikuwa na majukumu mengine spesheli ya kutekeleza kando na ya nyumba na angeelezwa na Bw Noor mwenyewe majukumu hayo ambayo yaliishia kuwa ya kumwosha maiti.

Akisimulia kwa machungu ya kusitisha mpigo wa moyo, Bi Owuor alisema aliwajibikia kazi ya kunadhifisha mwendazake wa kiume ambaye hakufahamu asili yake wala ukoo kila siku saa nne asubuhi.

 

Kazi ya siku 40

“Bw Noor alinichukua na kunipeleka chumba maalum na kuniamrisha nivute kitanda kisha nikaenda nyuma na nikakanyanga maiti. Maiti huyo alikuwa amekunjwa, nilishtuka sana ila alinielekezea bunduki na akanieleza kila kitu kisha hiyo ikawa kazi yangu kwa siku 40 kabla ya kukataa siku saba za mwisho,” akasimulia Bi Owuor.

Vile vile mwandada huyo alipewa maagizo ya jinsi ya kuchanganya kemikali ya kuosha madirisha kwa maji kisha kuitumia kumng’arisha marehemu.

Akiendeleza masimulizi yake, Bi Owuor alikumbuka jinsi mwanaume aliyefahamika tu kwa jina ‘daktari’ alivyofika kwa tajiri kila Jumanne na Ijumaa kumdunga sindano marehemu ili kuuzuia mwili kuharibika.

Vile vile alishangaa jinsi bosi wake alivyokuwa akitoa pesa kutoka kwa kitanda alikowekwa maiti huyo kila siku saa nane.

“Bosi wangu akitoka Isili mimi ndiyo tena na mvuta maiti kisha anatoa pesa. Zilikuwa pesa mpya, mamia tano, elfu moja, elfu tano. Nimepesa mpya unaweza fikiri zimetoka kwa benki na hakuna coins,” akaongeza.

Hata hivyo maajabu ya Musa ni kwamba tajiri huyo hakumpokeza mfanyikazi wake hata peni moja kwa kufanya kazi hiyo ya kuogofya kwa siku 40 na la kutamusha zaidi ni kufunguka kwa Bi Owuor kuwa bwenyenye huyo alijaribu kumdhulumu kimapenzi kisha alipokataa alifukuzwa bila malipo.

 

Kufinywa sehemu nyeti

“Alianza kunifinyilia kidole kwenye sehemu yangu ya siri usiku wa manane wakati faimilia yake ilikuwa imelala. Nilipiga kelele ndipo mkewe akaamka na kuja kuniuliza kilichootokea. Kama njia ya kufuta usemi wangu, Bw Noor alianza kunipiga na kunitupa nje nisijue pa kuelekea usiku huo,” akasimulia Bi Owuor ambaye alikesha kwenye baridi usiku huo.

Alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Pangani na cha kushangaza ni kwamba maafisa hao walifahamiana na Bw Noor na wakaishia kumfungia kwenye seli kisha kumwaachilia baadaye.

Kufika kwake kituo cha polisi cha Parklands na Mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa polisi kilimsaidia kumfungulia Bw Noor mashataka katika mahakama ya Kibera. Bw Noor hata hivyo aliwaachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 na tangu wakati huo kesi hiyo imekuwa ikiahirisha bila sababu.

Kupata haki kwake kumesalia ndoto kuu.

You can share this post!

Deacons East Africa kuwekwa katika usimamizi

Mwenyekiti wa MWA akejeli majigambo ya Matiang’i eti...

adminleo