• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Rafael Varane wa Kangemi anayetamani kuisakatia Chelsea

Rafael Varane wa Kangemi anayetamani kuisakatia Chelsea

Na PATRICK KILAVUKA

KUWA mwanasoka mtajika kunahitaji kujitolea mhanga maanake usipomakinika utasababisha masihara  na timu yako kuwa motoni kuadhibiwa mpira wa ikabu au tuta kisha matumaini ya timu kutumbukia nyongo baada ya nyavu kutikiswa.

Isitoshe, ikiwa ni fainali mashabiki huudhika na kukubebesha msalaba kando na kukulaani. Kumbuka aliyekuwa kipa wa Liverpool Loris Karius alipoiletea Liverpool balaa baada ya masihara yake kuipa Real Madrid ubingwa wa UEFA msimu wa 2017/2018.

Lakini mlinda ngome akiwa makini na kufuata mashauri ya kocha wake, hujifunga kibwebwe na kudhibiti mchezo wa wachezaji hasimu kwa kusoma mchezo wao kisha kuwazidi maarifa, kama afanyavyo kipa wa sasa wa Liverpool, Alisson Becker.

Huo ndio mtazamo chanya wa mwanadimba beki wa kulia Kevin Lisaka (pichani juu), 20, wa timu ya WYSA United ambayo inapatikana Kangemi, Kaunti ya Nairobi.

Timu hii ilikuwa inashiriki ligi ya Kaunti, Shirikisho la Soka Kenya FKF Tawi la Nairobi Magharibi na kuibuka ya pili bora msimuni kisha kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Kanda Nairobi West Regional League NWRL msimu ujao.

Lisaka alijiunga na timu hii akiwa chini ya miaka kumi na miwili kisha kuichezea kwa miaka miwili kabla kusajiliwa na timu ya Shangilia ya wasiozidi miaka kumi na minne Chini ya kocha Juma.

Aliisakatia kabumbu kwa miaka mitatu akiwa angali mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Old Kihumbuini, Kangemi hadi alipojiunga na shule ya upili.

“Niliitolea huduma zangu kwa moyo wa dhati. Wakati tulikuwa tumefunga, nilikuwa ninapata nafasi zaidi ya kufunguka kisoka. Niliichezea pia shule hadi viwango vya juu japo nilipofika kidato cha pili, wazazi walinitaka nizingatie masomo zaidi hali ambayo ilitatiza uchezaji wangu kwa kiasi,” aeleza mwanasoka huyu ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Matioli, Kaunti ya Kakamega.

Hata hivyo, alijikakamua kuzingatia kauli yao japo msukumo wa kipawa chake ulimpelekea kuvalia jezi tena akiwa kidato cha tatu.

Kuanzia wakati huo hadi sasa anapojiandaa kwenda kusomea taaluma ya teknolojia ya mawasiliano (IT), guu lake la dhahabu linazidi kuchongwa kustahamili dhoruba ya kabumbu kufaa timu.

“Baada ya kumaliza masomo ya shule ya upili, nimekumbatia talanta yangu ya soka kwa moyo wangu wote kwani nia yangu ni kuendeleza kipaji changu ambacho kimekita mizizi katika ukoo kwa sababu mjomba wangu Isaac Atundoli alikuwa mwanakandanda,” adokeza lisaka na kuongezea kwamba Mjomba wake aliichezea timu ya Kangemi United nafasi ya beki wa kulia ambayo ninaimiliki kikosini.

Mwanasoka huyu anasema kile ambacho kimemsukuma kuzingatia soka ni ushauri wa makocha na kufadhiliwa masomo na kuimarisha elimu yake kwa kufanya vyema. Fauka ya hayo, amekuwa na matumaini katika maisha kwani, angekipuuza kipaji chake, labda hangefika alikofika kimasomo na pia hangetalii sehemu mbalimbali za nchini.

“Ningepuuza ushauri wa mkufunzi wangu Turncliff Asibella ambaye hadi sasa ananishikilia mkono na kocha Juma wa timu ya Shangilia pamoja na kutilia maanani uchochezi wa mzazi wangu, baada ya kumshawishi kuhusu nia yangu ya kukichochea zaidi kipawa licha ya msimamo wake wa awali wa kutilia maanani masomo kuliko talanta, naona kama singefua dafu, “anafichua Lisaka.

Anasema baada ya kutambua umuhimu wa kipaji chake, mzazi alisawazisha mawazo yake na kuanza kumsapoti na vifaa vya michezo na hata kugharamia usafiri, wakati timu yao inaende kucheza michuano ya mbalimbali na eneo anakokaa na kumfanya apige moyo konde kuendeleza hatua zake katika kufikia ufanisi wa taaluma ya soka.

Tangu timu yake ya WYSA ianze kushiriki ligi ya  FKF Kaunti, Tawi la Nairobi Magharibi, mchezaji huyu amekuwa akishirikishwa kikosini kutokana na tajriba yake kwani, kocha wake Asibela amekuwa akimwekea matumaini makubwa kucheza katika nafasi ya beki nambari mbili. Na kwa kweli amekuwa akiitambisha timu kwa kufunga mkanda wa safu hiyo na kuondoa balaa kwenye msambamba.

Kocha wake anasema, yeye ni mwanakabumbu asiyetaka mzaha ngomeni. Anajituma na anapodhibiti boli huwa si rahisi kuiachilia hadi apeane pasi au autume mbele kwa minajili ya kusaka magoli. Isitoshe, huwa mchezaji anayetumia maarifa kukabili wapinzani.

“Tangu nimjengee msingi wa kandanda akiwa mdogo, nimekuwa nikiuelewa udhaifu wake hatua kwa hatua na kuurekebisha na sasa ninajivunia soka yake kwani, amekuwa mchezaji ambaye niko radhi kumfunza na kumchezesha. Pamoja na hayo, ni myenyekevu na hupenda kudumisha nidhamu ya hali ya juu, ” asema kocha huyo ambaye amemfunza mbinu za kimsingi za kucheza soka na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza ambacho kitakuwa kikisukuma gurudumu la ligi ya Kanda ya Nairobi Magharibi NWRL.

Mwalimu huyo soka ana matumaini makubwa kwamba endapo ataenda kwa majaribio bila shaka ana uwezo wa kuonesha utajiri wa kipaji chake ambacho kinanawiri.

Mwanasoka Kevin Lisaka akifunzwa mbinu za kukabili hasimu na kocha wake Turncliff Asibela.Picha/Patrick Kilavuka

“Lisaka ni mchezaji anayependa kuuwiana vyema na wachezaji wengine na ninatumai majaliwa akipata nafasi katika vilabu vikuu nchini ataweza kupiga gozi sawasawa, ” anakiri kocha huyo na kumpongeza kwa kuwa mwanasoka ambaye huwahimiza wanasoka wengine kikosini washinde wasishinde!

Kando na hayo, anasema uelewa wake wa kandanda umeifanya kazi yake ya kumnoa kwa rahisi na ushirikano wa bega kwa bega na wazazi wake umepeleka umepalilia hatua kadhaa kitalanta .

Shabiki wake Christian Kariba anasema alimjua mwanasoka huyu tangu akiwa shule ya msingi na ni mchezaji wa kujituma sana akiwa uwanjani.

Haogopi kukabiliana na wapinzani na huwatia wachezaji wa kikosi chake moyo kusaka ushindi au kucheza kadri ya uwezo wao. Hata hivyo, angependa kunarai azidishe maarifa ya kuvizia ili, aendelea kuwa beki moto wa kuotewa mbali.

Lisaka anakariri kwamba mechi ambayo ilikuwa yenye Changamoto ligini ilikuwa ile walishindwa na Uthiru Vision wakati wa ufunguzi wa Ligi ya Shirikisho la Soka Kenya FKF Kaunti NWCL kwani walipoteza 2-0.

Ingawa hivyo, angependa watie bidii ya mchwa mazoezini kuhakikisha kwamba watabeba timu msimu ujao.

Mchezaji ambaye humfurahisha kutokana na uchezaji wake ni Erick “Marcello” Ouma mchezaji wa zamani wa timu ya Gor Mahia ambaye sasa anakicheza Klabu ya Vasalund IF, Uswizi na difenda Mfaransa Raphael Varane wa Real Madrid.

Je, angependa kuchezea timu gani katika ulimwengu wa soka?

Anasema itakuwa furaha ilioje kuvalia jezi ya mabingwa wa KPL Gor Mahia na Chelsea ya ughaibuni!

You can share this post!

Rubani alala na kupita uwanja wa kutua

iPhone ni za wanawake maskini, wanaume mabwanyenye hutumia...

adminleo