Michezo

VIWANGO VYA FIFA: Harambee Starlets wazidi kuporomoka

December 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA inazidi kuporomoka katika Viwango vya Ubora vya Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) vya wanawake baada ya kuteremka nafasi sita hadi nambari 135 katika viwango vipya ambavyo vilitangazwa Desemba 7, 2018.

Harambee Starlets, ambayo ilikosa Kombe la Afrika (AWCON) lililoandaliwa nchini Ghana kutoka Novemba 17 hadi Desemba 1 baada ya Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) kuitema na kuipa Equatorial Guinea tena tiketi, ilikuwa imeteremka nafasi sita viwango bora vilivyotangazwa mara ya mwisho mnamo Septemba 28. Inamaanisha kwamba Kenya imeshuka nafasi 12 katika matangazo mawili yaliyopita ya viwango bora.

Mara ya mwisho warembo wa kocha David Ouma walisakata mechi ni Novemba 3 walipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Black Queens ya Ghana katika mechi ya kirafiki katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

Timu zote mbili zilikuwa zinatumia mchuano huo kujipima nguvu kabla ya kuelekea Ghana kwa Kombe la Afrika. Hata hivyo, Kenya iliachwa na mshangao pale ilipofungiwa nje ya mashindano hayo siku saba kabla ya mashindano kuanza baada ya CAF kurejesha Equatorial Guinea mashindanoni licha ya kuwa Kenya ilikuwa imeshinda kesi dhidi yake ya kutumia mchezaji asiye wa nchi hiyo kwa mechi za kufuzu. Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limeshtaki CAF katika mahakama ya kusikiza kesi za michezo (CAS) likisaka haki.

Ethiopia inasalia timu inayoorodheshwa juu katika viwango bora vya wanawake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Waethiopia wameshuka nafasi sita hadi nambari 116 duniani. Nambari mbili Cecafa ni Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFA) ambalo linashikilia nafasi ya 131 baada ya kuteremka nafasi sita. Kenya ni nambari tatu ikifuatiwa na Rwanda (chini nafasi sita hadi nambari 137) na Uganda ambayo imerushwa kutoka 135 hadi 141.

Marekani ni nambari moja duniani katika orodha hii ya mataifa 152. Waamerika wamekwamilia nafasi hiyo. Wanafuatiwa na Wajerumani ambao bado wanashikilia nafasi ya pili.

Ufaransa imeruka juu nafasi moja hadi nambari tatu ikisukuma Uingereza nafasi moja chini hadi nambari nne. Canada na Australia hazijasonga kutoka nafasi za tano na sita mtawalia nayo Netherlands imepaa nafasi tatu hadi nambari saba. Japan imeshuka kutoka nafasi ya saba hadi nambari nane, Uswidi inasalia ya tisa nayo Brazil inafunga 10-bora.

Mabingwa wa Afrika Nigeria wanasalia katika nafasi ya kwanza barani Afrika, lakini wako chini nafasi moja hadi nambari 39 duniani. Cameroon na Afrika Kusini zimeimarika kwa nafasi tatu na mbili hadi nambari mbili na tatu mtawalia barani Afrika na 46 na 48 duniani. Ghana imetupwa chini nafasi tatu hadi nambari 50 duniani.

Ivory Coast ni ya tano Afrika na 68 duniani baada ya kupaa nafasi moja. Equatorial Guinea ndiyo imeangukia pua zaidi katika viwango hivi. Imeteremka nafasi 16 hadi nambari 70 duniani.