UDAKU: Size 8 aelezea alivyokwea mlima wa shida hadi akawa mdosi
NA SINDA MATIKO
KWA sasa nguvu zake nyingi kazielekeza kuendeleza injili, lakini kabla ya hapo Size 8 alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki waliotetemesha chati za burudani hapa nchini.
Hata hivyo, hadi akaishia kuwa staa, Size 8 anasema, ilikuwa ni safari ya misukosuko kibao ambayo wakati mmoja ilimwacha akiwa amefilisika vibaya.
Akitokea familia ya kimaskiani, mwanamuziki huyu ambaye majina yake halisi ni Linet Masiro Munyali, anasisitiza kuwa anaelewa bayana maana ya kukosa na ndio sababu alijitosa kwenye muziki kujaribu kubadilisha maisha baada ya familia yake kushindwa kumudu karo za kumpeleka Chuo Kikuu.
Alipoachilia hiti yake ya kwanza ‘Shamba Boy’, kwa kusaidiwa na produsa veterani Clemoo, Size 8 ambaye kipindi hicho alikuwa na miaka 21 tu, alianza kuona tupesa tukiingia.
“Shamba Boy ilipoanza kuchezwa kwenye redio, nazo shida zangu kibao zikaanza kupungua. Nilianza kuitiwa shoo ndogo ndogo tu ambazo hazikuwa na mtaji mkubwa ila nilishuruku maana sikuwa nimewahi kuona pesa nyingi kama zile.
“Nilikuwa nalala chini, nikanunua kitanda, nilikuwa napika kwa jiko la mkaa, nikanunua jiko la gesi, nilikuwa naishi kwenye chumba kimoja nikahamia nyumba yenye chumba kimoja cha kulala. Zilikuwa ni hatua ndogo ndogo zenye mashiko,” anasema.
Baada ya kuona Shamba Boy imefanya vizuri, Size 8 anasema aliamua kucheza kamari kwa kuwekeza fedha zake zote alizokuwa amekusanya kama akiba kuachilia kibao kingine.
“Nilikuwa nimekusanya zikawa ni Sh230, 000. Nikaamua kucheza pata pote na fedha hizo. Nilichofanya mwanzo ni kununua makaa ya kutosha, maharagwe na ndengu na kuweka nyumbani kisha nikalipa kodi ya miezi mitatu mbele. Fedha zote zilizosalia, nikaamua kurekodi wimbo ‘Vidonge’ pamoja na kushuti video yake kwenye studio ya Ogopa DJ.
Baada ya kutumia fedha zote hizo nilifilisika. Ila mambo yalikuwa mawili hapa, kama wimbo huo utaishia kuwa hiti basi mambo yatanyooka na kama utafeli basi narudi kwenye umaskini wangu,” anasimulia. Wimbo ulipotoka tu, Size 8 anasema maisha yake yalibadilika kabisa na kumfanya tajiri.
“Miezi miwili tu baada ya wimbo kutoka, maisha yangu yalibadilika kabisa. Niliangukia dili kubwa kubwa ambazo sikuwahi kufikiria zingeweza kutokea maishani mwangu. Nilisaini dili ya Safaricom Live. Nikasaini dili ya kuigiza kwenye kipindi cha Citizen TV kilichoitwa Mashtaka, nikafanya matangazo kibao ya kibiashara za runingani, nikahusika kwenye shindano la Sakata Dance Challenge. Hela zikaanza kuungia tena kwa fujo. Nasema hili bila hata ya kupepesa macho, naamini kipindi hicho nilikuwa miongoni mwa wasanii wachache sana waliokuwa wakilipwa kiasi kikubwa cha pesa Afrika Mashariki,” anajigamba.
Mpunga ulipoingia kwa kishindo, maisha ya Size 8 nayo yakaanza kubadilika kwa mpigo. “Nilinunua gari langu la kwanza tena kwa kulipia pesa taslimu sio mkopo wala nini. Nikahama toka nyumba ya chumba kimoja hadi Penthouse pale South B sasa nikawa naishi kwenye nyumba yenye vyoo kadhaa na vyumba vya kulala. Maisha yakabadilika na kuwa matamu sana,” anaongeza.