Man U wakaribisha Arsenal katika kona ya majonzi ya kutandikwa
NA MWANGI MUIRURI
Mashabiki wa Arsenal wameingia Mwaka Mpya 2024 katika Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa na taharuki kuu kuhusu ndovu kuanguka kutoka juu ya mti na kulemaa.
Hii ni baada ya kupokea kichapo cha pili mfululizo Desemba 31, 2023 ambapo ilichapangwa magoli 2-1 na timu ya Fulham.
Magoli kutoka Jimenez dakika ya 29 na De Cardova Reid katika dakika ya 59 yalifutilia mbali shangwe ya Arsenali katika dakika ya tano kutoka kwa kifaa matata, Bukayo Saka.
Timu ambayo juzi ilikuwa imejipa matumaini kwamba 2023/24 ndio msimu wao kuchukua taji la ligi hii kwa sasa shaka ndizo nyingi hata ya uwezekano wa kumaliza ndani ya nne bora ukiwa hafifu.
“Sitaki hayo maneno kabisa. Mambo ya Arsenal yamenifika koo kwa mahangaiko. Mbona wakanipa matumaini makuu ya kuingia kutazama kabumbu nikiwa mwingi wa bashasha ya kushangilia ushindi halafu ghafla mimi najipata nikilia?” akasema Bi Cecilia Kamau, 24, ambaye ni mwanafunzi wa taasisi ya kimatibabu ya Murang’a.
Katika mji wa Murang’a tulikumbana na mashabiki wengine waliokataa katakata kujibu swali la jinsi walivyokuwa wakihisi kutokana na adhabu hiyo iliyowashusha hadi nafasi ya nne katika jedwali.
Iwapo itateleza katika mechi itakayofuata ya 21, basi itashuka tena hadi nafasi ya tano iwapo Tottenham itaendelea kupata ushindi.
Lakini katika mji wa Sabasaba tulikumbana na shabiki sugu wa Arsenal kwa jina David Saka Njoroge aliyesema kwamba “ni hali ya kabumbu ambapo gozi likikukataa dunia hupasuka”.
Bw Njoroge alisema “kwa kweli tumesambaratika katika muundo na ueledi lakini ni kwa muda tu tutarejea”.
Hata hivyo, Sammy De Gea Gitau wa Manchester United alishabikia kichapo cha Arsenal akikitaja kama malipo ya ujeuri.
“Sisi tukikaangwa huwa mko na kiherehere sana na huwa mnaudhi. Sasa mmejipata katika hali yetu na nashabikia…Karibuni tulie pamoja,”akasema.
Mnamo Ijumaa, Man United walikuwa wametandikwa magoli 2 kwa 1 na Nottingham Forest.