Gachagua asimulia jinsi aliponea kufungwa hadi 2073
NA MWANGI MUIRURI
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua Januari 1, 2024 akiwa katika jela kuu la King’ong’o amefichua kile alichosema ni njama iliyokuwa imesukwa ya kumfunga gerezani miaka 50, huku pia akitetea dhifa zake za mchele na nyama Mlima Kenya.
Bw Gachagua alisema kwamba ni utamaduni usioeleweka na watu wa magazeti na mitandao ya kijamii kwamba Waafrika hujadiliana katika mazingira ya mlo.
Alisema ataendelea mbele na kuwaandalia watu wake mlo wa aina hiyo, akiwa pia amewapangia wafungwa hao mlo sawa, akisimulia jinsi aliponyoka kuwa mahabusu.
“Nilikuwa na pesa yangu kima cha Sh12.6 bilioni. Idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) iliyokuwa imekolea dhuluma ikasema nimeiba hiyo mali,” akakariri.
Aliongeza kwamba DCI ilimpangia njama ya kumshtaki kwa makosa ya wizi “lakini wakiitishwa mlalamishi hawakuwa naye”.
Alisema kwamba kesi hiyo ilikuwa ya kipekekee “kwa kuwa kortini walikuwa wakisukuma majaji wanifunge bila ushahidi”.
Aliongeza kwamba “wakiulizwa pesa imeibwa wapi, kutoka kwa nani, kwa benki gani, akiwa na bastola wapi…hawakuwa na jibu”.
Bw Gachagua alisema kwamba “hatimaye baada ya mahakama kugundua ukosefu wa ushahidi uliokuwa unazingira kesi hiyo, majaji waliafikiana kwamba kesi hiyo irushwe hadi baada ya uchaguzi”.
Hapo ndipo, akasema, aliponyoka kitanzi cha jela “kwa kuwa leo hii ningekuwa mmoja wenu hapa tukitembelewa na maafisa wa serikali mimi nikiwa ndani kwa miaka 50”.
Angefungwa miaka hiyo na rufaa zikataliwe, Gachagua angetoka jela akiwa na miaka 107.
Alisema kwamba hata kinara wa Azimio Bw Raila Odinga alifika katika Kaunti ya Nyeri kuchapa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 “na akatangaza hadharani kwamba wangechukua serikali mimi ningeishia kuwa mahabusu”.
Aliongeza kwamba kauli hiyo ilipewa nguvu na aliyekuwa mbunge wa Kieni wakati huo Bw Kanini Kega “aliyesema ningefungiwa King’ong’o kwa kuwa kwetu ni Nyeri ili jamaa na marafiki wawe wakija kuniletea uji”.
Alisema njama hiyo ilimpata alikamatwa mara kwa mara na hata akazoea maisha ya kulala ndani ya seli juu ya simiti bila gondoro wala blanketi.
“Ni kwa sababu hiyo ambapo nimekuja hapa kuwapa motisha kwamba haya mnayopitia ni ya muda na mtaishia kutoka na mjiunge na wananchi wengine huko nje,” akasema.