Uhuru alivyoruka mtego hatari wa serikali na Mungiki uwanjani Kabiru-ini
NA MWANGI MUIRURI
Imefichuka kwamba Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliruka mtego mkali wa serikali—ikidaiwa kushirikiana na aliyekuwa kinara wa Mungiki Maina Njenga—wa kumwangazia kama aliyekuwa na nia ya kufufua genge hilo na kulipa mamlaka ya juu Mlima Kenya.
Kwa mujibu wa dokezi kutoka idara za kiusalama, njama hiyo kali ilikuwa imesukwa na kuzinduliwa Mei, 2023 na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya walio ndani ya serikali ya Kenya Kwanza, hasa wale wa eneo la kati.
“Kwa kuwa kundi hilo linaogopwa na kuchukiwa katika Mlima Kenya, kulibuniwa mpango wa kukabiliana na Uhuru ambaye alikuwa akinukuliwa na ripoti za ujasusi (NIS) kama mmoja wa aliyekuwa akifadhili maandamano ya Azimio dhidi ya serikali. Mpango huo uliambwa kwa kuzinduliwa kampeni za kumhusisha Uhuru na kundi hilo haramu la Mungiki,” akasema mmoja wa mdokezi wetu.
Katika hali hiyo, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kinara wa wengi bungeni Bw Kimani Ichung’wa na Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro walizindua semi za hadharani za kumwangazia Uhuru kama mfadhili wa Mungiki, wakiungwa mkono pembeni na wanasiasa wengine katika Kaunti za Mlima Kenya.
Itakumbukwa kwamba watatu hao katika mikutano kadha ya kisiasa na ya hadhara walitangaza kwamba Uhuru alikuwa mfadhili wa Mungiki wakidai analenga kutumia genge hilo kuzua msukosuko wa kisiasa eneo la Mlima Kenya.
“Ili njama hiyo ipenye mashinani, ni lazima aliyekuwa kinara wa Mungiki Bw Maina Njenga angehusishwa kwa kuwa alikuwa mrengo wa Azimio na ndipo alianza kusakamwa akikamatwa na kufikishwa mahakamani,” asema mdokezi wetu katika wizara ya usalama wa ndani.
Tulifahamishwa kwamba awamu ya pili ya mpango huo ilikuwa ya kumsaidia Bw Njenga kuandaa mikutano ya hadhara na awe akisema Uhuru alikuwa akimuunga mkono na tayari kulikuwa na mpango wa kumpisha yeye (Njenga) kama msemaji wa jamii za Mlima Kenya.
“Enda umwambie Njenga afunguke roho na aseme wazi kuhusu tukio la Septemba 15, 2023 ambapo alidai alitekwa nyara akiwa mjini Kiambu na kisha akaachiliwa baada ya siku nne. Muulize alikuwa wapi, alikutana na kina nani, wakapanga nini na hatimaye akaanza kuonekana akisaka maridhiano na serikali ya Rais William Ruto lakini akizidisha njama za kusema alikuwa mwaniaji wa msemaji wa Mlima Kenya akiungwa mkono na Uhuru,” tukagutushwa.
Mnamo Septemba 22, 2023 ndio siku inayosemwa kuwa ya kipekee ambapo Njenga alihudhuria mazishi ya aliyekuwa shujaa wa Mau Mau katika Kaunti ya Nyeri Bi Muthoni Kirima na ambapo muombolezaji mashuhuri alikuwa ni Gachagua.
“Mimi sina shida na Gachagua au mwingine yeyote katika siasa za Mlima Kenya. Mimi niko Azimio kama msimamizi wa masilahi yenyu na tunafaa kuungana pamoja. Hata mkitaka nivae kofia ya siasa za hapa nitaivaa sina shida na sina vita. Tuache vita, tuungane na Rais Mstaafu Kenyatta amewasalimia na amesema tuko pamoja,” akasema Bw Njenga katika hotuba yake.
Akimjibu, Gachagua alisema “kabla hawa wakane historia yao chafu ya ghasia na ujambazi hakuna siku tutaketi nao meza moja”.
Dokezi zetu kutoka idara za kiusalama zilituelekeza katika mkutano mkubwa wa Njenga wa Oktoba 7, 2023 katika uwanja wa Kimorori ulioko katika eneo bunge la Maragua hatua chache tu kutoka makao makuu ya kiusalama ya Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini.
“Enda urejelee mikanda ya mkutano huo uniambie kama kulikuwa na tashwisi ya serikali kuunga mkono mkutano huo kikamilifu. Ugoro ulitumika, nyimbo za Mungiki zikasheheni, vijana wakatoa hakikisho kwamba wamerejea na hata baadhi ya vyombo vya habari vikasaidiwa kuwa na usalama ndio habari hizo ziwafikie wengi,” akasema afisa mmoja mkuu wa usalama wa Murang’a.
Katika mkutano huo, Njenga alikariri kwamba alikuwa aandae mkutano mkubwa Desemba 31, 2023 wa kufunga mwaka katika uwanja wa Kabiru-ini ulioko kaunti ya Nyeri na ambapo alidai Uhuru angefika na amtawaze kuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya.
Hapo ndipo kambi ya Uhuru ilianza kuwa na shaka na mikutano hiyo ya Njenga na mnamo Novemba 30, 2023 aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni pamoja na mwanablogu wa Jubilee Pauline Njoroge walilalama hadharani kuhusu mtindo wa Njenga kurejelea jina la rais huyo mstaafu katika mikutano yake.
Mwenyekiti wa baraza la wazee Bw Wachira Kiago pia alisema kwamba “wadhifa huo ambao Njenga anasema atatwikwa na Uhuru uko na utaratibu wake na kwa sasa hakuna hafla ambayo tumepanga ya kumteua mwingine wa kurithi majukumu hayo kutoka kwa rais huyo mstaafu”.
Bw Kiago alisema “nia ya Njenga ni ya kumharibia Uhuru jina na kumwingiza katika siasa za hadaa na ujambazi kwa nia ya kumfanya apoteze umaarufu Mlima Kenya”.
Idara za usalama zinasema kwamba “kabla ya tetesi hizo za kina Kioni, Njoroge na Kiago, Uhuru alikuwa akipanga kuhudhuria mkutano huo wa Kabiru-ini”.
Lakini baada ya kuingiwa na shaka na kupata ushauri kutoka kwa wandani wake ndani ya vitengo vya kiusalama, Uhuru aliafikia uamuzi wa kutofika katika uwanja huo.
“Serikali ambayo hapo mbeleni ilikuwa ikimpa nafasi Njenga kuandaa mikutano pasipo matatizo ikamgeuka na kuharamisha mkutano wa Kabiru-ini ili sasa kujiangazia kama iliyokuwa haina nafasi ya kurejea kwa kundi hilo katika siasa na jamii ya Mlima Kenya,” akasema afisa mmoja.
Aliongeza kwamba iwapo Uhuru angeamua kufika katika mkutano huo, haungezimwa na serikali lakini punde tu ukimalizika kulikuwa kumepangwa vikao 20 na vyombo vya habari katika Kaunti 15 na pia mikutano mingine 12 eneo la Mlima Kenya kukemea ‘hatua ya Uhuru kuteua Mungiki’ kuwa kinara ndani ya siasa za eneo hilo.
Rais mstaafu Uhuru akawa ameruka mtego huo huku nao walio ndani ya serikali sasa wakibidi kurejea tena katika ususi wa njama nyingine mbadala.