Michezo

#HonoluluMarathon: Wakenya wavuna mamilioni

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Titus Ekiru na Vivian Jerono Kiplagat walijizoelea Sh2,561,500 kila mmoja baada ya kunyakua mataji ya wanawaume na wanawake ya Honolulu Marathon nchini Marekani mnamo Desemba 9, 2018, mtawalia.

Ekiru aliongezwa Sh307,410 kwa kukamilisha kilomita 42 za wanaume chini ya saa 2:10. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 26, ambaye alishinda Mexico City Marathon nchini Mexico mwezi Agosti, alikata utepe kwa saa 2:09:01, sekunde 34 nje ya kasi ya juu kuwahi kushuhudiwa katika mji huu. Mkenya mwenzake Lawrence Cherono alinyakua taji la mwaka 2017 kwa saa 2:08:27.

Wakimbiaji 27, 000 waliingia makala haya ya 46, ingawa 25,059 ndiyo walishiriki. Walioshiriki walistahimili upepo mkali uliochangia pakubwa katika kasi ya chini iliyoshuhudiwa. Hali ya anga ilikuwa tulivu mwanzo na mwisho wa mbio pekee.

Hata hivyo, Ekiru na Kiplagat walikosa ushindani katika kilomita 21 za mwisho. Ekiru na Mkenya mwingine Vincent Yator walikuwa mbele pekee yao katika kitengo cha wanaume kufikia kilomita ya 21. Walikuwa bado pamoja kufikia kilomita 25 kabla ya Ekiru kumuacha Yator na kisha kufungua mwanya wa dakika mbili na nusu alipofika kilomita ya 30.

Vivian Jerono Kiplagat alijizoelea Sh2,561,500 baada ya kunyakua taji la wanawake ya Honolulu Marathon nchini Marekani mnamo Desemba 9, 2018. Picha/ Hisani

Kilomita tano za mwisho zilikuwa ngumu kwa Ekiru kutokana na uchovu, ingawa mwanya aliokuwa amefungua ulikuwa mkubwa sana kupunguzwa na nambari mbili. Ekiru, hata hivyo, hakuweza kuvunja rekodi ya Cherono na kukosa bonasi ya kuweka rekodi mpya ya Sh1,024,700.

Mkenya Reuben Kerio alimpita Yator na kumaliza katika nafasi ya pili kwa saa 2:12:59 naye Yator akaridhika katika nafasi ya tatu (2:15:31).

Mwamerika Donn Cabral alifunga mduara wa nne-bora (2:19:16). Kiplagat,30, alikuwa mbele ya wenzake kwa dakika moja kufikia kilomita ya 15 na kukimbia kilomita zilizobaki akiwa pekee yake na wanaume mbele akikata utepe kwa saa 2:36:22.

Nafasi ya pili ilinyakuliwa na Mkenya Sheila Jerotich (2:42:09) naye Mjapani Eri Suzuki akaridhika katika nafasi ya tatu (2:47:53).  Malkia wa Honolulu Marathon mwaka 2014 na 2015 Joyce Chepkirui, ambaye alikuwa ameapa kujishindia taji hili tena, hakumaliza.

Wanaume wa Kenya wameshinda Honolulu Marathon mara 12 mfululizo tangu mwaka 2007. Kenya imeshinda kitengo cha kinadada tangu mwaka 2014.