Bambika

Faith Lukosi atia wivu wanawake wa Kenya kwa kudekezwa na mumewe hadharani

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

WAKILI na mkurungezi wa Youth Enterprise Development Fund Faith Norah Lukosi, amemsifu mumewe, Bw Donald Juma, akitaka ulimwengu kufahamu kuwa ni mtu anayemjali sana na ni baraka maishani mwake.

Bi Lukosi ameambia Taifa Leo kuwa anafurahia hatua ya mumewe kumwaminia na kumwelewa kutokana na shughuli zake za kila siku.

“Nashukuru mume wangu kwa kunielewa na kunipa nafasi akijua kwamba kazi yangu inahitaji muda mwingi. Kwa mwezi utapata naondoka nyumbani kila siku. Mara nina mkutano Mombasa kwa juma moja na hata kabla nirejee nyumbani, nafahamishwa kuna mkutano mwingine Naivasha… Yaani mara nyingi sipatikani nyumbani kabisa. Mkutano mmoja utachukua wiki mbili hivi, ule mwingine siku nne,” akasema Bi Lukosi.

Wakili huyo alisema kuwa ndoa yao kuimarika, ni kutokana na wao wawili kuelewana akisema urafiki wao ulianza mwaka 2018.

“Mimi na mume wangu husaidiana. Aidha, ndoa yetu imejengwa kwa msingi wa kuaminiana na uwazi,” alisema Bi Lukosi.

Katika makaribisho ya Mwaka Mpya wa 2024, Bw Juma ambaye anatoka kijiji cha Khachonge eneobunge la Kabuchai, alimmiminia sifa mkewe kupitia chapisho kwa ukurasa wa Facebook.

Bw Juma aliandika akisimulia jinsi ambavyo Faith Norah amekuwa baraka maishani mwake.

“Ulikuja maishani mwangu kama baraka. Umeyafanya maisha yangu kuwa mazuri na ya kutamanika. Tunapoanza mwaka mpya, endelea kunitia moyo na kuniunga mkono. Ahsante kwa msaada wako mpenzi,” aliandika Bw Juma.

Baba huyo wa watoto wanne alithibitisha kuwa Bi Lukosi mwenye umri wa miaka 32, amekuwa nguzo ya usaidizi kwa familia yake yote.

“Ahsante Mungu kwa kunipa familia nzuri zaidi, mwanamke anayejali, mwenye upendo, anayeelewa, mwanamke mchapakazi zaidi, mwanamke mrembo kuliko wote duniani, mwaminifu, na zaidi ya yote, mwanamke aliyebarikiwa zaidi. Faith Norah Lukosi, mimi nimebarikiwa sana kuwa nawe maishani mwangu. Ahsante kwa kuwavisha wazazi wangu zawadi za gharama kubwa zaidi ulizowatunuku, mpenzi. Ahsante kwa kumfanya kukhu (nyanya) yetu Victoria atabasamu. Ahsante kwa yote ambayo umefanya,” akaongezea.

Faith Norah ni mkurungezi wa shirika la Youth Enterprise Development Fund. Aidha, aliwahi kuwania kiti cha Usenata katika Kaunti ya Nairobi kupitia chama cha Jubilee mwaka wa 2022 lakini hakufaulu.