Habari za Kitaifa

Korti yazima mawakili kuponyoka na Sh74m

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imekanyagia mawakili wawili breki kulipwa kitita cha Sh74.3 milioni na mwekezaji kutoka Rwanda Desire Muhinyuza.

Akiamuru mawakili Omwanza Nyamweya na Ivy Ateko Ingati wasilipwe mamilioni hayo ya pesa, Jaji Alfred Mabeya alisema Jumatano “wawili hao hawakufanyia kazi kampuni ya Stay Online Limited (SOL) iliyokuwa inang’ang’aniwa na Bw Muhinyuza na mfanyabiashara Bw Kirimi Koome.”

Jaji huyo alifutilia mbali agizo Sh74.3 milioni zihamishwe kutoka akaunti ya SOL katika benki ya United Bank of Africa (UBA) tawi la Westlands, Nairobi ziwekwe katika akaunti ya wakili Ingati.

Jaji huyo alisitisha agizo kutekelezwa kwa agizo la Jaji Josphine Wayua Wambua Mong’are la Oktoba 30, 2023, kwamba Sh74.3 milioni ziwekwe katika akaunti ya Bi Ingati kutoka akaunti ya SOL.

Mawakili wa Bw Muhinyuza, Mabw Danstan Omari, Aranga Omaiyo, na Shadrack Wambui, pamoja na Bi Sophie Nekesa walipinga kesi ya malipo ya Sh74.3 milioni ya mawakili hao wawili wakisema maafikiano kati yao na SOL kuhusu malipo hayo yanapotosha.

Bw Omari alieleza jaji Mabeya kuwa mkataba wa malipo uliowasilishwa mbele ya jaji Mong’are na mawakili hao wawili Bw Omwanza na Bi Ingati ulikuwa na nia ya kuilaghai SOL pesa za wateja wake.

Jaji Mabeya alisema mawakili hao wawili hawakutetea SOL bali walimwakilisha Bw Koome katika kesi aliyoshtakiwa ya kula njama za kuilaghai kampuni hiyo Dola 2.6 milioni (Sh400 milioni).

Bw Omwanza na Bi Ingati wanamwakilisha Bw Koome katika kesi hiyo inayosikilizwa na hakimu mkazi Bw Ben Mark Ekhubi.

Kesi hiyo ya ufisadi dhidi ya Bw Koome itasikilizwa Februari 6, 2024.

Bw Koome alishtakiwa kufuatia malalamiko ya Bw Muhinyuza kwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwamba Bw Koome alilaghai umiliki wa kampuni ya SOL na anapania kutumia kwa mambo yake pesa za wateja zinazofika Sh400 milioni.

Maafisa wa DCI walipata agizo kubana pesa hizo Sh400 milioni.

Mnamo Desemba 27, 2023, jaji Mabeya alimtangaza Bw Muhinyuza kuwa mmiliki wa kampuni ya SOL.

Raia wa Rwanda na mwekezaji Desire Muhinyuza akiwa katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi mnamo Desemba 27, 2023, ambapo mahakama ilithibitisha ndiye mmiliki wa kampuni ya Sh400 milioni ya Stay Online Ltd ambayo alizozania na Mkenya Kirimi Koome. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Mnamo Desemba 28, 2023, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia mawakili wa serikali Bi Dorcus Rugut na James Gachoka, aliamuru Bw Muhinyuza arudishiwe pesa hizo Sh400 milioni kwa vile Mahakama Kuu ilimtambua kuwa mwenye kampuni ya SOL.

Jaji Mabeya alisema katika uamuzi wake kwamba Bw Koome alikuwa amejipatia umiliki wa SOL kwa njia ya ufisadi.

Jaji Mabeya alisema Bw Koome alikataa kufichua mmiliki halisi wa SOL alipoisajili Aprili 14, 2023.

Bw Koome alikuwa ameteuliwa na mseto wa kampuni za SOL kusajili tawi la kampuni hiyo humu nchini mnamo Aprili 1, 2023.

Jaji Mabeya alisema Bw Koome alijitambua kwa msajili wa kampuni kuwa mmiliki wa SOL, Kenya.

Mahakama ilielezwa na Bw Muhinyuza kuwa bodi ya SOL, Rwanda iliidhinisha Dola 129,000 (Sh19 milioni) zitumwe kwa akaunti ya SOL, Kenya kuzindua huduma zake.

SOL huuza bidhaa katika mtandao.

Mbali na Rwanda, SOL inahudumu nchini Canada, Estonia, Zambia, Uganda, Tanzania, na Kenya.

Jaji Mabeya alielezwa Sh400 milioni zilizokuwa katika akaunti ya UBA, Westlands jijini Nairobi ni za wateja na wala si za Bw Koome.

Wakati kesi ya mzozo wa umiliki wa SOL, Kenya ilipokuwa inaendelea, mawakili Bw Omwanza na Bi Ingati waliwasilisha ombi mbele ya Jaji Mong’are na kudai wao na SOL wameafikiana kitita cha Sh74.3 milioni kitengwe kugharimia ada yao ya kuiwakilisha kesi hiyo.

Bw Omari alisema taarifa hiyo kwa jaji Mong’are ilikuwa ya kupotosha na kuomba mawakili hao wazimwe kujinufaisha kwa pesa hizo kwa njia isiyo halali.

Jaji Mong’are aliagiza mzozo huo wa ada ya mawakili wa Sh74.3 milioni uamuliwe na jaji Mabeya aliyesikiliza kesi ya umiliki wa SOL.

Jaji Mabeya alitenga Februari 16, 2024, siku ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo waliyoishtaki SOL mawakili hao Omwanza na Ingati.