Simiyu mwingi wa matumaini Shujaa itatamba licha ya matokeo duni
Na GEOFFREY ANENE
LICHA ya Kenya Shujaa kuanza Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 vibaya sana, kocha wa zamani Innocent “Namcos” Simiyu ana matumaini makubwa na timu hiyo.
Shujaa, ambayo ilipata kocha mpya Paul Murunga mwezi Oktoba baada ya Simiyu kukataa kuomba kuendelea na kazi hiyo, ilishinda mechi yake ya kwanza kwa kuchapa mabingwa wa Afrika Zimbabwe 31-19 katika nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16 hapo Desemba 9 katika duru ya Cape Town Sevens nchini Afrika Kusini.
Mabingwa hawa wa zamani wa Afrika walikuwa wamepoteza mechi nane mfululizo tangu msimu uanze mjini Dubai mnamo Novemba 30. Walipoteza dhidi ya Scotland (35-14), Ufaransa (21-17), Fiji (43-12), Uhispania (26-19) na Japan (26-19) mjini Dubai na kumaliza katika nafasi ya 15 (mkiani) kwa alama moja hapo Desemba 1.
Vichapo vilichacha katika duru ya pili mjini Cape Town mnamo Desemba 8-9 pale Shujaa ilipepetwa na Uingereza (29-12), Fiji (38-7) na Ufaransa (19-12) kabla ya kuonja ushindi wa kwanza kwa kuzima Zimbabwe 31-19 na kisha kulaza Wales 33-26 katika fainali ya kupata nambari 13 na 14.
Shujaa ilikamilisha ziara ya Cape Town katika nafasi ya 13 kwa alama tatu. Kwa sasa, Waafrika hawa wanashikilia nafasi ya 14 kwa alama nne, moja mbele ya Japan, ambayo inashikilia nafasi ya 15 na katika hatari ya kutemwa kutoka ligi hii ya duru 10.
Katika mahojiano Jumatatu na Simiyu, ambaye aliongoza Shujaa kujiandikia historia ya kumaliza Raga ya Dunia kwa zaidi ya alama 100 tangu mwaka 1999 baada ya kuvuna alama 104 msimu 2017-2018, amesema anaamini Shujaa ilijitahidi kadri ya uwezo wake katika Dubai Sevens na Cape Town Sevens.
“Naamini vijana walijitolea kwa moyo wao wote. Nimeridhishwa sana na ari ya wachezaji wapya, hasa (Daniel) Taabu, (Johnstone) Olindi na Vincent (Onyala). Naona maisha ya baadaye yatakuwa sawa. Hata hivyo, kuna kazi kubwa Shujaa inastahili kufanya kabla ya duru ijayo, hasa jinsi ya kunyaka mipira inapoanzishwa na pia kuimarisha ulinzi,” amesema nahodha huyu wa zamani wa Shujaa na pia timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande alamaarufu Simbas.
Kenya imekutanishwa na wafalme wa Raga ya Dunia ya msimu 2017-2018 Afrika Kusini katika Kundi C kwenye duru ya Hamilton Sevens itakayofanyika nchini New Zealand mnamo Januari 26-27, 2019. Itakutana pia na Scotland na Ufaransa mjini Hamilton katika kundi hilo.
Kuhusu Hamilton Sevens mwaka 2019, Simiyu amesema, “Tumetiwa katika kundi nzuri la Hamilton Sevens na ninaamini kwamba vijana watapata matokeo mazuri bora tu wajiandae vyema. Tunawaunga mkono asilimi 100 na kuwatakia kila la kheri.”
Kundi A linajumuisha Fiji, Australia, Argentina na Wales. Marekani, Uingereza, Samoa na timu alikwa ziko katika Kundi B. Wenyeji New Zealand watalimana na Uhispania, Canada na Japan katika Kundi D.
Msimamo wa Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 baada ya duru ya Dubai na Cape Town:
Marekani (alama 38)
New Zealand (37)
Fiji (35)
Uingereza (30)
Afrika Kusini (29)
Australia (25)
Scotland (20)
Argentina (18)
Uhispania (17)
Samoa (15)
Ufaransa (12)
Canada (10)
Wales (5)
Kenya (4)
Japan (3)
Zimbabwe (2).