LSK yamtaka Ruto akome kuishambulia mahakama
NA CHARLES WASONGA
CHAMA cha Mawakili Nchini (LSK) kimemkosoa vikali Rais William Ruto kwa kudai majaji ni wafisadi huku kikimtaka kuwasilisha ushahidi kuhusu uovu huo kwa Tume ya Idara ya Mahakama (JSC) ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwenye taarifa mnamo Jumatano, Rais wa LSK Eric Theuri amemtaka kiongozi wa nchi kuwa mstari wa mbele kuheshimu sheria na Katiba na uhuru wa Idara ya Mahakama kwa ujumla.
“Rais akome kuwachafua majina majaji wote na badala yake atumie mkondo wa sheria kupinga maamuzi ya majaji hao husika ambayo hajaridhika nayo. Hii hatua ya kuchochea umma dhidi ya majaji ni hatari kwa thamani ya Katiba yetu na heshima na uaminifu kwa mfumo wetu wa kisheria,” akaeleza.
Bw Theuri alimkumbusha Rais Ruto kwamba Idara ya Mahakama ndio mtetezi na mlinzi wa Katiba ya Kenya na kwa miaka mingi “imesimama kidete kudhibiti hulka ya serikali kutumia vibaya mamlaka yake.”
“Mheshimiwa Rais anafaa kufahamu kwamba ni mahakama iliyosambaratisha juhudi za serikali iliyopita za kulazimisha mageuzi ya Katiba kinyume na matakwa ya wananchi. Ilifaulu kuzima mpango uliofahamika kama Building Bridges Initiative (BBI),” Bw Theuri akaongeza.
Rais huyo wa LSK alisema hayo Jumatano baada ya Rais Ruto kudai kuwa majaji huhongwa na watu fulani kuzima miradi na mipango ya serikali yake.
Akiongea katika hafla ya mazishi eneo la Njabini katika Kaunti ya Nyandarua mnamo Jumanne, Kiongozi wa Taifa alisema kuwa serikali yake itakoma kuheshimu maagizo ya mahakama kwa sababu majaji wanahongwa kuvuruga mipango ya serikali.
“Tunaheshimu Idara ya Mahakama lakini ukiukaji wa sheria unaoendeshwa na majaji wafisadi sharti ukome nchini au tutaukomesha kwa vyovyote vile,” Dkt Ruto akasema.
Alikuwa amehudhuria mazishi ya babake Seneta wa Nyandarua John Methu, Mzee Michael Maigo.
Dkt Ruto aliapa kuwa miradi ya barabara katika eneo la Nyandarua iliyositishwa na agizo la mahakama itaendelea “wapende wasipende”.
Kando na LSK, kauli ya Rais Ruto pia imekosolewa vikali na Chama cha Majaji na Mahakimu na viongozi wa matabaka mbalimbali.