Habari za Kitaifa

SRC yazima tena ulafi wa wabunge

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA DAVID MWERE

TUME ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) imepinga mswada unaopendekeza kuwa wabunge waliohudumu kwa muda wa chini ya miaka 10 walipwe pensheni.

Aidha, mswada huo unapendekeza kuwa wabunge waliohudumu kwa hadi miaka mitano walipwe malimbikizi ya pesa za kuhudumu afisini (gratuity).

Kwenye taarifa iliyotumiwa Bunge la Kitaifa, SRC inasema Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Pensheni ya Wabunge ya 2023 inakiuka sheria na katiba.

Afisa Mkuu wa SRC Bi Anne Gitau alionya kuwa pensheni ni manufaa kutokana na uajiri na hivyo hukadiriwa na SRC.

“Kwa hivyo, mswada wowote unaopendekeza kubadili malipo ya pensheni sharti uafiki mamlaka ya SRC yaliyoko kwenye Katiba,” Bi Gitau akasema.

“Mswada huo unaingilia wajibu wa SRC. Kwa mswada huo unaolenga kubadilisha malipo ya pensheni ya maafisa wakuu katika bunge unakiuka Katiba na hivyo ni batili,” anaongeza.

Kulingana na kipengele cha 230 (4) (a) cha Katiba SRC ndio asasi ya kipekee ya serikali iliyo na mamlaka ya kukadiria na kubadilisha viwango vya mishahara na manufaa mengine yanayolipwa maafisa wakuu na maafisa wa umma.

Kifungu cha 8 cha Mswada huo kinalenga kuondoa sehemu ya 7 ya Sheria ya Pesheni ya Wabunge na badala yake kuweka maneno “mtu ataweza kupokea malipo ya kuhudumu afisini baada ya kukoma kuwa Mbunge na amehudumu kwa miaka mitano au chini ya miaka hiyo.”

Mswada huo pia unapendekeza kuwa Mbunge ambaye amehudumu kwa zaidi ya muhula mmoja anaweza kuamua kulipwa malipo ya kuhudumu afisini “badala ya” pensheni baada ya muhula “ambao mbunge huyo alikuwa akihudumu wakati huo.”

Mswada huo vile vile unasema kuwa ikiwa baada ya kupokea malipo hayo, mbunge huyo ataamua kulipa michango ya pensheni, atahitajika kulipa pesa zote alizolipwa pamoja na riba ya asilimia 3 kila mwezi kwa miaka 15 kuanzia siku ambayo aliamua kuanza kuchangia pensheni.

Hata hivyo, SRC inasema kuwa pendekezo hilo linatoa taswira kwamba ni wabunge waliohudumu kwa miaka mitano au chini ya miaka hiyo ambao wanafaa kupokea malipo ya kuhudumu afisi.

Aidha, linaashiria kuwa wabunge waliohudumu kwa chini ya miaka 10 wanaweza kulipwa pensheni.

Badala yake SRC inataka kifungu hicho kiondolewe kutoka kwa Mswada huo na kuwekwa kile kinachosema wabunge waliohudumu kwa angalau muhula mmoja walipwe aidha pensheni au malipo ya kuhudumu.

Wakati huu, wabunge waliohudumu kwa angalau mihula miwili ndio wamehitimu kulipwa malimbikizi ya Sh7 milioni kama malipo ya kuondoka, kabla ya kutozwa ushuru wa asimilia 30 na malipo ya Sh118, 000 kila mwezi kama pensheni.

Wale ambao wamehudumu kwa miaka isiyotimu miaka 10 hulipwa malipo ya kuhudumu ambayo hukadiriwa kwa kiwango cha asilimia ya mishahara yao kila mwaka wa kuhudumu.

Aidha, wao hurejeshewa michango yao ya pensheni ya kila mwezi pamoja na asilimia 60 ya mchango huo kutoka kwa serikali.