Makala

Watu ni kupambana na ‘githeri rasta’ Januari

January 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LABAAN SHABAAN

KILA msimu wanabiashara wa mikahawa huibuka na mbinu nyingi za kuandaa mapochopocho nafuu kwa wanachuo wanaotafuta chakula bora kisicho ghali.

Baada ya kuvuma kwa chakula maarufu kwa jina ‘ugali pambana’ hoteli ya Lakers Dishes iliyoko Kahawa West eneobunge la Roysambu Kaunti ya Nairobi, imebuni Githeri Rasta.

Ni chakula kinachoongeza ladha kwenye pure (githeri) na kuifanya tamu kwa mionjo ya nyama ya kuku ama ng’ombe.

Mmiliki wa hoteli hiyo Lenson Munene anaeleza chakula hiki ni mseto wa tambi (noodles ama spaghetti) na githeri.

Hoteli ya Lakers Dishes inayopendwa na wanachuo kwa ubunifu wa kuandaa vyakula mbalimbali. PICHA | LABAAN SHABAAN

Wengine hukiita ‘Ng’ang’a’ kuashiria mchanganyiko wa spaghetti na pengine kwa kuwa walaji wa githeri hung’ang’ana wakati githeri ina mahindi magumu.

Jina rasta linatokana na umbo la tambi kuwa kama misokoto ya nywele maarufu kama rasta.

“Tulishirikiana na kampuni za kuuza tambi ili kuvumbua chakula hiki kuongeza mvuto wa githeri na wateja wameongezeka huku wengi wakitaka kujua ni chakula gani,” alieleza katika mahojiano na Taifa Leo.

“Siku ya kwanza kuuza githeri rasta tuliuza makumi ya sahani na tangu hapo wateja wanazidi kuongezeka,” akaongeza.

Bw Munene ambaye pia ni mlaji wa mlo huu alisema maswali mengi yameibuka mitandaoni watu wakitaka kukijua chakula hiki.

Kupitia apu kama vile ya glovo, Lakers Dishes inalenga kuongeza githeri rasta kwenye menu kwa sababu ya kukua kwa hitaji la mapochopocho haya.

Wengi wa wateja wa chakula hiki ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, wakazi wa Wadi ya Kahawa West, Githurai, Ruiru wengine wakiwa wapitanjia.

“Wanaoagiza githeri rasta kwa mara ya kwanza kupitia mitandao huwa tunawalipisha bila ada ya usafiri na kupunguza bei kwa asilimia 10,” alieleza Bw Munene ambaye anatumia mbinu mbalimbali kupanua mtandao wa wateja wake.

Nilitembea katika mikahawa kadhaa eneo la soko la KM ambapo The Lakers Dishes ipo kukagua menu zao bila kupata mlo wa githeri rasta ambao unauzwa kwa Sh80.

“Nadhani sisi ndio wabunifu zaidi katika mtaa huu ukizingatia uandaaji wa vyakula.

Hii ni sababu wateja wengi wanatupenda na imebidi tujaribu kuwafurahisha,” alisema Bw Munene akiongeza kuwa hoteli hiyo huwa na uwezo wa kubeba wateja zaidi ya 200 ambapo wengine hupanga foleni wakisubiri muda wa kuhudumiwa.

Tulizungumza na baadhi ya wanafunzi ambao hupenda kilaji hiki.

“Aliyebuni githeri rasta alifanya vizuri sana! Mimi hujibebea avokado na kuongeza rojo ya nyanya kuzidisha utamu,” alisema mwanafunzi Kate Achieng.

Mwanafunzi mwingine wa KU anayeishi KM, Joe Meto, alisema akitania: “Hiki ndicho chamcha changu. Hii rasta hufanya githeri kushibisha tumbo vizuri na sishikwi na njaa kwa muda mrefu.”

Kama sili githeri rasta mchana, wakati mwingine nachangamkia ugali pambana,” Meto aliongeza.

Ugali pambana ni mlima wa ugali ulioandaliwa kwa minofu ya mifupa pamoja na supu.

Katika hoteli hii, chakula hiki huuzwa kwa wateja ambao hawawezi kumudu bei ya nyama.

Kwa hivyo huuzwa kwa Sh100 huku nyama kwa ugali ikiuzwa kwa angalau Sh150 ama Sh200.