CDF isipodunda kwa akaunti zetu katika saa 48 patachimbika, Wabunge waonya serikali
BAADHI ya wabunge kutoka eneo la Magharibi sasa wanaitaka serikali kutoa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) ndani ya saa 48 ili wanafunzi wapokee basari kabla shule kufunguliwa Jumatatu.
Mbunge wa Kiminini Kakai Bisau alielezea hofu kuwa huenda wanafunzi kutoka jamii maskini wakakosa kurejea shuleni ikiwa serikali itaendelea kuchelewesha pesa hizo.
“Hali ni mbaya zaidi hapa mashinani. Wabunge wanawekewa presha na wananchi wanaosaka basari. Wamekuwa wakija nyumbani mwetu kila asubuhi wakitafuta msaada ila hatuna pesa kwenye akaunti zetu za CDF,” alisema jana Bw Bisau.
“Ikiwa hizo pesa hazitatolewa ndani ya saa 48 zijazo basi watoto wengi kutoka jamii maskini hawataripoti shuleni Jumatatu,” akaonya.
Alikuwa akizungumza baada ya kufungua rasmi daraja la Wekhonye linalounganisha maeneo ya Hilario na Nabiswa katika eneobunge lake la Kiminini.
Bw Bisau alimtaka Rais William Ruto kuingilia kati suala hilo ili “watoto werevu kutoka familia maskini wapate nafasi ya kusoma”.
Mbunge wa Luanda Dick Maungu aliunga mkono kauli hiyo akisema kuwa serikali inafaa kuipa elimu kipaumbele kwani ni haki ya kikatiba.
“Sawa na eneobunge la Kiminini ambalo halijatoa pesa za basara, eneobunge la Luanda pia halijatoa pesa zozote kwa sababu hazipo. Watoto kutoka familia maskini ambao tumekuwa tukiwadhamini wanahitaji pesa hizo kwa dharura,” Bw Maungu akaeleza.
Mbunge huyo alimtaka Waziri wa Fedha, Profesa Njuguna Ndung’u, kutimiza ahadi aliyotoa kwa wabunge mwezi jana kabla yao kwenda likizo ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, kwamba angetuma pesa za CDF baada ya majuma mawili.
Mnamo Desemba 5, 2023 wawakilishi hao wa maeneobunge walivuruga shughuli za Bunge wakaondoka ukumbini kwa hasira wakilalamikia kucheleweshwa kwa mgao wa fedha za CDF.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti, Ndindi Nyoro, aliahidi kuwa serikali ya kitaifa itatoa pesa za basari katika hazina ya CDF “kabla ya wanafunzi kuripoti shule kwa muhula wa kwanza”.
“Serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha wanafunzi wanaotegemea pesa za CDF kugharamia masomo yao hawatakosa kufika shuleni kuendelea na masomo,” alisema mbunge huyo wa Kiharu jana.
“Juzi, serikali ilitoa Sh3.5 bilioni pesa za mpango wa masomo bila malipo kwa shule zote za msingi na za upili za umma. Ninahakikishia wanafunzi kutoka familia maskini pamoja na wabunge wenzangu kwamba serikali itatoa pesa za CDF kabla ya shule kufunguliwa Jumatatu,” Bw Nyoro alisisitiza.
Shule zinafunguliwa rasmi kuanzia Jumatatu kwa muhula wa kwanza kwenye kalenda mpya ya masomo mwaka huu.
Nao wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wataanza kuwasili shuleni mnamo Januari 15.