Michezo

Jinsi mashindano ya waheshimiwa yalivyovutia mashabiki kuliko ligi za FKF

January 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHINDANO maalum ya soka yaliyodhaminiwa na watu binafsi majuzi katika sehemu mbalimbali kote nchini wakati wa shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya yatakumbukwa kwa kuvutia mashabiki wengi kuliko ligi za kawaida zinazoendeshwa na Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

Wakati wa mashindano hayo katika viwanja vya Bukhungu Stadium mjini Kakamega, Jomo Kenyatta ya Kisumu, Raila Odinga Homabay, Mumias Complex, Mutunini High School (Nairobi) pamoja na Siagonjo ya Busia miongoni mwa vingine imebainika kwamba vijana wengi wamebahatika kupata timu kubwa za kuchezea ligini kuanzia mwaka huu mpya wa 2024.

Baadhi yao wameitwa kujiunga na shule maalum za kunoa vipaji katika mataifa ya kigeni kwa ufadhili huku wakiendelea na masomo ya kawaida.

Kulingana na taarifa za waandalizi wa mashindano hayo, wengi wa wachezaji hao walipatikana kutoka shule za sekondari baada ya kuvutia maskauti waliokuwa miongoni mwa mashabiki waliohudhuria mashindano hayo.

Itakumbukwa kwamba wakati wa mashindano ya shule za sekondari yaliyofanyika hapo awali katika kaunti ya Kakamega mwezi Agosti, Adrin Kibet, Amos Wanjala na Alvin Kasavuli waling’ara katika kikosi cha St Anthony ya Uasin Gishu na baadaye kujiunga na chuo cha Nastic Soccer Academy (NSA), Tarragona nchini Uhispania baada ya kupata ufadhili.

Chipukizi mwingine aliyefaidika baada ya kumalizika kwa mashindano ya shule ni Louise Ingavi, mshambuiaji matata ambaye sasa yuko Montiverde Soccer Academy nchini Amerika kunoa kipaji chake mbali na kuendelea na masomo ya kawaida.

Kibet, Wanjala, Kasavuli na Ingavi walikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya iliyoshindwa na Uganda fainali na kumaliza katika nafasi ya pili katika mashindano ya CECAFA ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18.

Baadhi ya wachezaji wa Kakamega Homeboyz washerehekea baada ya kuchapa AFC Leopards 1-0 ugani Bukhungu na kutwaa Elijah Lidonde Cup. PICHA | HISANI

Kulingana na data za wachambuzi wa maswala ya kandanda nchini walioshuhudia mashindano yaliyomalizika majuzi katika Kanda za Magharibi na Nairobi, fainali za Elijah Lidonde Super Cup, Fernandes Barasa Super Cup, na John ‘KJ’ Kiarie Super Cup zilizofanyika Bukhungu Stadium na Mutuini High ndizo zilizovutia mashabiki wengi.

Kadhalika, utafiti umeonyesha kwamba mashabiki wengi walitaka mechi hizo ziendelee lakini imekuwa vigumu kutokana na ratiba ya FKF ambayo imerejea baada ya mapumziko ya wiki mbili kwa ajili ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Mbunge wa Shinyalu Fred Ikana (kushoto), Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, na Gavana wa Kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa wakiwa katika uwanja wa Lugala Sports Complex, Jumatano wakati wa fainali za Fred Ikana Cup. Lyon FC kutoka Wadi ya Isukha Kusini iliipiga Shisokoro kutoka Wadi ya Murhanda 1-0 kubeba taji hilo. PICHA | HISANI

Maendeleo na ufanisi mkubwa unaendelea kushuhudiwa. Wachezaji Chris Kaloti, Kelly Madada, Dennis Biketi, na Mark Shaban ambao walikuwa wakichezea timu ya Shule ya Upili ya Shanderema kutoka Kaunti ya Kakamega, sasa wamesajiliwa na klabu ya Green Commandos inayoshiriki Ligi ya FKF Divisheni ya Kwanza.

Klabu hiyo inadhaminiwa na wanafunzi wa zamani wa Shule ya Kitaifa ya Kakamega High.

Duru zinasema wengi wa wachezaji hao wa Green Commandos wanawindwa na klabu yenye historia ndefu, AFC Leopards.