Habari za Kitaifa

MCK yalaani shambulio dhidi ya wanahabari jijini Nairobi

January 6th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

BARAZA la Vyombo vya Habari nchini (MCK), Jumamosi lililaani vikali shambulio lililotekelezwa dhidi ya wanahabari kwenye operesheni iliyoongozwa na Halmashauri ya Kitaifa ya Kukabiliana na Matumizi ya Mihadarati (NACADA) jijini Nairobi.

Wanahabari hao kutoka mashirika ya KBC, Nation Media Group (NMG), The Standard, na runinga ya Citizen, walishambuliwa na mabaunsa wa kilabu kimoja jijini Nairobi, ambako maafisa wa NACADA waliwapata baadhi ya watu wakivuta Shisha Ijumaa usiku.

Baadhi ya wanahabari hao walipata majeraha mabaya, wengine wakapoteza simu huku vifaa vyao vya kazi vikaharibiwa.

Baraza lililaani vikali shambulio hilo, likilitaja kama uingiliaji wa haki ya wanahabari kutekeleza majukumu yao.

“Kwa kuwalenga wanahabari ambao walikuwa wakitekeleza majukumu yao, lengo kuu la washambuliaji hao lilikuwa kuvizuia vyombo vya habari kutekeleza jukumu lake la kuwafahamisha Wakenya kuhusu masuala yanayohusu maisha yao,” likaeleza baraza hilo kwenye taarifa.

“Baraza linashinikiza wanahabari wote waliojeruhiwa au kupoteza vifaa vyao vya kazi kulipwa ridhaa na mmiliki wa klabu husika na watu waliowashambulia pia,” likaongeza.

Hata hivyo, liliwashukuru polisi waliofika katika eneo hilo haraka na kuwakamata washukiwa.

Baraza pia lilimrai Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuhakikisha kuwa wanahabari hao wamepata haki.

Chama cha Wanahabari Kenya (KUJ) pia kililaani shambulio hilo.

Operesheni hiyo iliongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA, Bw Anthony Omerikwa.