Michezo

Mgombea wa urais FKF ahofia maisha yake ushindani ukitiwa doa

January 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirika la Extreme Sports, Hussein Mohammed, anahofia usalama wa maisha yake siku chache tu baada ya kudhulumiwa na watu waliomzuia kuingia katika uwanja wa Raila Odinga kushuhudia fainali ya Kombe la Gavana wa Kaunti ya Homa Bay.

Kulingana na Bw Mohammed ambaye ni mmoja wa wagombeaji wakuu wa kiti cha Urais wa FKF, watu waliomvamia walidai kwamba walifanya kitendo hicho kufuatia maagizo kutoka kwa afisa mmoja wa ngazi ya juu kwenye kamati kuu ya FKF.

Bw Mohammed ambaye kwa miaka mingi amekuwa mstari wa mbele kuimarisha soka kuanzia mashinani, amesema amekuwa akitishiwa mara kwa mara na watu wasiojulikana.

“Vitisho hivyo vinahusiana na uchaguzi unaokuja,” akasema Bw Mohammed.

Katika mahojiano na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Ijumaa jijini Nairobi, Bw Mohammed ambaye hajatangaza rasmi kujitosa uwanjani kuwania kiti hicho, alisema kuwa ana wasiwasi kuhusu maisha yake na ya wanaomuunga mkono katika juhudi za kuwania wadhifa huo.

Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari katika mkutano huo, alisisitiza kwamba vitisho hivyo havitamzuia kutimiza majukumu yake ya kurudisha hadhi ya soka nchini.