Ndindi Nyoro ashauri wabunge wasitumie mgao wa NG-CDF kukarabati vyoo vya shule
NA SAMMY WAWERU
WABUNGE hawapaswi kutengea vyoo vya shule fedha za ujenzi kupitia mgao wa ustawishaji maeneobunge (NG-CDF), na badala yake waelekeze pesa hizo kwa miradi mingine muhimu, mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ameshauri.
Bw Ndindi anasema, vyoo vya shule vinapaswa kukarabatiwa endapo vitashinikizwa na visa vya dharura.
Kulingana na mbunge huyu ambaye utafiti unaonyesha amekuwa akiongoza kimaendeleo tangu achaguliwe, hali ya vyoo katika shule zote nchini ni mbaya na kuvitengea mgao wa Hazina ya NG-CDF kutakwamisha utekelezaji wa miradi muhimu.
“Hakuna shule ya umma, hasa shule za msingi, ambayo haihitaji choo. Kila shule unayozuru, vyoo vina shida. Unaweza ukatumia fedha za CDF kukarabati vyoo hadi ziishe,” akasema Bw Nyoro.
Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto, majuzi alitembelewa na wabunge kutoka maeneo tofauti nchini kusoma jinsi yeye hutumia hazina ya NG-CDF kutekeleza maendeleo.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza 2017, na anasema ni aibu kwa mbunge au yeyote anayehusishwa naye kusimama kanisani na kuambia watu alivyofanya maendeleo kwa kukarabati vyoo shuleni.
“Ni aibu kujipigia debe jinsi ulivyofanya maendeleo kwa kukarabati vyoo vya shule. Ukarabati wa vyoo, utekelezwe ikiwa ni kisa cha dharura,” akashauri wabunge waliomzuru kwa minajili ya mafunzo.
Baadhi ya wabunge pia walituma wawakilishi wao kusomeshwa jinsi Bw Nyoro amefanya maendeleo eneobunge la Kiharu.
Novemba 2023, mbunge huyo wa chama tawala cha UDA aliorodheshwa na shirika la utafiti la Infortrak kama mbunge mchapakazi bora zaidi nchini.
Alitwaa nafasi ya kwanza, akipewa asilimia Nyoro 70, huku akifuatwa kwa karibu na mwenzake wa Kangema, Bw Peter Irungu (asilimia 68).
Tafiti hizo za Infortrak, pia zilitaja wabunge watano kushikilia nafasi tatu, nao ni; Paul Mwirigi wa Igembe Kusini, Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati), Christopher Wangaya wa Kwisero, Robert Mbui (Kathiani) na Peter Kaluma wa Homa Bay Mjini.
Aidha, tano hao walizoa asilimia 66 kila mmoja.
Ndindi Nyoro anasema kufanikisha azma ya NG-CDF, ni muhimu mbunge awe na malengo na pia ashirikishe kupitia utoaji maoni wapigakura wa eneobunge lake.
“Kwa mfano, katika eneobunge la Kiharu hufanya mikutano na wenyeji katika kila kijiji kuwaomba mawaidha na kutaka kujua maendeleo wanayotaka,” akasema Bw Ndindi.
Kila mwaka, kila eneobunge hupata angalau wastani wa Sh157 milioni (NG-CDF) kutoka kwa serikali kuu.
Hata hivyo, mgao huo unatolewa kulingana na idadi ya watu katika eneobunge na kiwango cha maskini, hivyo vikiwa baadhi ya vigezo vinavyotumika kuusambaza.
Kenya ina jumla ya maeneobunge 290.