Wavulana wawika kwa Alama za A na E huku wasichana wakikamata C na D nyingi
Na MWANGI MUIRURI
Wavulana ndio walivuna kwa wingi alama za juu na pia za chini katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) 2023 wakipata (A) 825 na wenzao wa kike wakiambulia 391.
Vilevile, katika alama ya E, wavulana walijipa zao 28,214 nao wasichana wakiwa na chache kidogo, 19, 960 katika matokeo.
Ni katika tu alama za C+, C, C-, D+ na D ambapo wasichana waliwalemea wavulana katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne wa 2023, yaliyotangazwa na Waziri Ezekiel Machogu.
Katika alama ya A-, wavulana 4, 472 waliipata huku wenzao wa kike wakijipa zao 2, 782.
Wasichana 7,708 walipata alama ya B+ huku wavulana 10,370 wakiipata. Katika alama ya B- ni wavulana 30,521 waliivuna huku wasichana 28, 993 wakifanikiwa kuinyaka.
Alama ya B ilivunwa na wavulana 19, 822 huku wasichana 16, 906 wakiidaka.
Katika alama ya C+ ni wavulana 38, 888 ambao waliivuna huku wasichana 39, 455 wakiipata. Mambo yalikuwa vivyo hivyo katika alama ya C ambapo wasichana 48, 411 dhidi ya wavulana 44, 201 waliipata.
Alama ya C- ilikuwa na wasichana 56,855 dhidi ya wavulana 50,616 nayo ile ya D+ ikivutia wasichana 66,032 dhidi ya wavulana 58, 974. Alama ya D ilinaswa kwa wingi na wasichana wakiwa 79,612 nao wavulana wakiivuna wakiwa 75,664.
Nayo alama ya D-ilishangiliwa na wavulana 86,429 dhidi ya wasichana 79, 432.
Hata hivyo, mifano ya walioanguka mtihani wa sekondari lakini wakaishia kuwa watu mashuhuri ilitolewa katika hafla hiyo ya Januari 8, 2024 katika shule ya Upili ya Moi Girls mjini Eldoret.
Kwa mfano, Mbunge mwanamke wa Uasin Gishu Bi Gladys Boss Shollei alikiri katika kikao hicho kwamba alipata alama ya chini zaidi enzi zake katika mtihani wa CPE lakini akaishia kuwa wakili, msajili katika mahakama kuu na kwa sasa mbunge ambaye pia ni Naibu wa Spika katika bunge la Kitaifa.
“Ningetaka mjue kwamba matokeo ya mtihani mmoja hayawezi kuamua hatima yako ya kimaisha. Kama taifa, tunafaa kushikana kuwaongoza watoto wetu kuzidi kupaa licha ya changamoto za matokeo ya mitihani,” akasema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika bunge la Seneti Bw Joe Nyutu alisema kwamba kuna shida kubwa ya elimu nchini kwa kuwa kuna ukosefu wa ajira.
“Nawashawishi wale watakaokosa nafasi katika vyuo vikuu wafikirie sana kujiunga na taaluma za kiufundi,” akasema.
Alisema kwamba nafasi za kazi kwa uchumi wa sasa zinaegemea kozi za kiufundi na kwa sasa serikali imepatia taasisi za kiufundi kipau mbele.
“Msiwe wa kurandaranda mitaani mkisema hakuna mianya ya kazi. Jiungeni na taasisi za kiufundi kwa kuwa serikali inatoa ufadhili wa Sh30,000 kwa kila mwanafunzi,” akasema.