Habari za Kitaifa

Waliodanganya kwenye KCSE walisaidiwa na wataalamu, ripoti yafichua

January 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

Watahiniwa 4,113 walioripotiwa kuhusika katika udanganyifu katika Mtihani wa KCSE wa 2023  walisaidiwa na wataalamu waliotwikwa jukumu la kushughulikia mitihani, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema.

Kati ya waliohusika, Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) lilifuta matokeo ya watahiniwa wanne baada ya kukamilisha uchunguzi.

Kulingana na waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, wanne hao walifanyiwa mitihani na watu wengine.

“Matokeo ya watahiniwa 4,109 waliosalia ambao walituhumiwa kujihusisha na dosari za mtihani yamezuiliwa kusubiri kukamilika kwa uchunguzi ndani ya muda wa siku 20 kuanzia leo,” alisema Machogu.

Baraza limepewa mamlaka kisheria, kushughulikia udanganyifu katika mitihani kwa kuzuia matokeo ya mtahiniwa au kituo chochote cha mitihani kinachoshukiwa kuhusika na ukiukaji wa utaratibu au utovu wa nidhamu kusubiri uchunguzi kukamilika.

Bw Machogu alisema kwamba wengi waliohusika na udanganyifu walisaidiwa na wataalamu waliopatiwa kazi ya kushughulikia mitihani.

“Inasikitisha kwamba wataalamu wachache walio na kandarasi bado wanasisitiza kuharibu mustakabali wa wanafunzi wetu kwa kuhusika katika makosa ya mitihani. Wataalamu mia moja na ishirini (120) walio na kandarasi waliripotiwa kuhusika katika kusaidia kutenda makosa ya mitihani. Hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Bw Machogu.

Walimu wakuu kadhaa walikamatwa kwa kushukiwa kuhusika na visa vya udanganyifu wakati wa mtihani wa KCSE mwaka jana.

Waziri alitangaza kuwa wizara imeunda jopo la kupokea malalamishi kuhusu matokeo ya mitihani.

Kwa hivyo, nawaomba Wakenya ambao hawajaridhika na michakato yoyote ya Baraza La Mitihani kutafuta suluhu kupitia jopo hilo,” alisema.