Habari za Kaunti

Arati ataka waliotibua mkutano wake wakamatwe

January 9th, 2024 2 min read

RUTH MBULA Na WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kisii Simba Arati sasa anataka polisi kuwakamata na kuwashtaki anaowaita wahalifu waliofyatua risasi hewani na kutawanya watu katika mkutano wa hadhara eneobunge la Mugirango Kusini.

Watu wanne walipata majeraha ya risasi huku wengine wakiuguza majeraha ya kupigwa kwa rungu, mapanga na kurushiwa mawe.

Kamanda wa Polisi Kisii Bw Charles Kases amesema uchunguzi kuhusu matukio hayo umeanza.

Gavana Arati anamlaumu mbunge wa eneo hilo aliye pia Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro na tayari ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kisii Central mjini Kisii.

Bw Arati anasema maisha yake yako hatarini.

Bw Osoro kwa upande wake anajiondolea lawama huku akimlamu gavana kwa yaliyotokea.

Gavana alikuwa amesimama katika soko la Nyakembene katika shughuli zake za kugawa fomu za basari wakati shambulio hilo lilitokea.

“Nilikamilisha shughuli ya kugawa fomu katika maeneo ya Chitago, Getenga na Moticho bila tatizo. Lakini nikihutubia wakazi Boikang’a, wahuni wa mbunge walifika na wakaanza kufyatua risasi. Walikuwa na angalau bunduki tatu aina ya AK 47,” akasema gavana Arati.

Video iliyonasa tukio hilo ilionyesha Bw Arati akihutubia mamia ya wakazi wa Nyakembene kabla ya watu wasiojulikana kufika hapo na kuanza kufyatua risasi kiholela, huku watu wakijaribu kadri ya uwezo wao kukimbilia usalama wao.

Pia katika video hiyo, mtu mmoja akiwa amevalia kiraia anaonekana akiwa na bunduki akitafuta watu wa kuwafyatulia risasi.

Ilibidi maafisa wa ulinzi wa Gavana kumkinga huku wakimpeleka kwa gari lake.

Lakini pia walirushiwa gesi ya kuwafanya watokwe na machozi.

Ilimlazimu Bw Arati kuondoka kwa gari lake na kujificha kwa shamba la mahindi.

Hali iliendelea kuwa mbaya, huku mawe yakirushwa kiholela.

“Miezi saba iliyopita kulitokea shambulio kama hilo katika mazishi Mugirango Kusini na polisi hawajamkamata yeyote kufikia sasa,” akalalama Bw Arati.

Lakini akijitetea, Bw Osoro alidai kwamba alikuwa katika eneo la Nyamarambe akipeana basari alipofahamishwa kwamba fujo zilitokea Nyakembene.

“Nilikuwa na shughuli nyingi ikiwemo kufanya uzinduzi wa barabara 24 katika eneobunge langu. Nilitaka kuzindua barabara ya Nyabisase-Nyakembene, lakini niliposikia kwamba gavana yuko upande huo, nilihisha wangu hadi katika eneo la kilomita moja kutoka alipokuwa,” akasema Bw Osoro.

Alidai kwamba timu yake ya kuasili kabla ya yeye mwenyewe ilishambuliwa na “watu wa gavana ambao walitwaa vitu vingi ikiwemo maikrofoni.”

“Watu wangu walikimbilia usalama wao na baadaye wakajipanga upya kuenda kudai vitu hivyo kutoka kwa watu wa gavana,” akasema, akifafanua kwamba hapo ndipo fujo zilichacha ambapo madereva wake wawili walijeruhiwa.

Alidai kwamba Bw Arati ndiye alipanga mashambulio na kisha akajifanya ndiye aliyekosewa.