Mvulana aliyeripoti shuleni Kanga High na sanduku tupu azoa B+
NA CHARLES WASONGA
MVULANA ambaye aliripoti katika Shule ya Upili ya Kanga, Kaunti ya Migori kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2020 akiwa na sanduku tupu na bila karo, amepata alama ya B+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023).
Levis Otieno Rabah, ambaye masomo yake yalifadhiliwa na wahisani kutokana na mapato duni katika familia yake, Jumatatu alileta tabasamu kubwa kwa familia hiyo.
Otieno aliandikisha matokeo mazuri katika masomo yote saba, huku alama ya chini kabisa ikiwa ni B- aliyopata katika somo la Kiingereza.
Matokeo ya mvulana huyo yalikuwa kama yafuatavyo: Somo la Kompyuta A, Jiografia A-, Kiswahili B+, Bayolojia B+, Fizikia B, Kemia B, Hisabati B kisha Kiingereza B-.
Madhila ya Otieno, ambaye alipata alama 390 katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE), yaliangaziwa kwa mara ya kwanza na runinga ya NTV.
Hii ni baada ya mvulana huyo kuripoti shuleni akiwa na sanduku tupu, na vipande viwili vya sabuni ya mti almaarufu sabuni ya kipande, ambavyo ndivyo wazazi wake walimudu kumnunulia.
Kutokana na umaskini, wazazi wake hawangeweza kumnunulia mahitaji mengine, kama vile sare na vitabu, pamoja na kumlipia Sh53,000 zilizohitajika kama karo yake kila mwaka.
Otieno aliwaambia wanahabari kwamba aliamua kuripoti shuleni bila karo na mahitaji mengine baada ya kuwasilisha maombi ya basari na kukosa kufaulu.
Mtangazaji na mcheshi (sasa Mbunge wa Lang’ata) Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o alijitokeza kumsaidia mvulana huyo kwa kumlipia karo ya miaka minne baada ya madhila ya Otieno kuzagaa mitandaoni.
Wahisani wengine waliofuatia walijitokeza na kumnunulia mahitaji mengine ya shule.
“Niliongea na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Kanga kwa njia ya simu. Nilimhakikishia kuwa nitalipa karo yote ya Otieno ambayo ni Sh53,000 kila mwaka,” Bw Jalang’o akaeleza wakati huo.