Makala

Ruto: Sina bajeti kuhonga majaji  

January 9th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto ameonekana “kuboresha” mashambulizi kwa Mahakama kufuatia Mpango wake wa Ujenzi wa Nyumba za Bei Nafuu kuyumbishwa na korti, sasa akisema hana bajeti yoyote kuhonga majaji.

Kulingana na kiongozi wa nchi, bajeti aliyo nayo ni ya kufanya miradi ya maendeleo kukuza Kenya.

Akizungumza Jumanne, Januari 9, 2023 Kapseret, Eldoret wakati wa uzinduzi wa msingi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, Dkt Ruto alisema kwa vyovyote vile hawezi akahonga Idara ya Mahakama ili kuruhusu maendeleo ya serikali yake kufanyika.

Kwenye mashambulizi yake, Rais alisema hawezi kuiga mkondo wa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta akidai Rais mstaafu huyo alikuwa na bajeti ya kuhonga majaji.

“Ati kuna watu wengine wanasema kwa sababu ile serikali nyingine (Jubilee) ilikuwa na bajeti ya kuhongana korti, nifuate huo mkondo. Wanasema niwe na bajaeti hiyo…Ati niwe na wakili kuhongana kortini. Mimi sina pesa za kuhonga mahakama. Pesa nilizo nazo ni za maendeleo,” Rais Ruto akaambia wakazi wa Eldoret, akizindua ‘jiwe’ la ujenzi wa nyumba za Pioneer, Kapseret, Uasin Gishu.

Chini ya utawala wa Serikali ya Jubille, Ruto alihudumu kama naibu wa rais.

Na badala yake, kiongozi wa nchi anasema atabadilisha Idara ya Mahakama iwe ikitoa huduma bila kuhongwa – akisisitiza, “Mahakama ni asasi ya serikali ambayo inapaswa kuhudumia Wakenya bila kupokea rushwa”.

“Huo uwendawazimu wa Mahakama kuhongwa nitausimamisha,” Dkt Ruto akaapa.

Rais amekuwa akishambulia Idara ya Mahakama hasa baada ya Mahakama Kuu Novemba 2023 kuharamisha Sheria ya Makato ya Ada za ujenzi wa Nyumba za Bei Nafuu.

Korti ilitaja makato ya asilimia 1.5 kwa mshahara wa mwajiriwa na kiwango sawa na hicho kuchangwa na mwajiri kugharimia mradi huo, kama haramu na ambayo yanakiuka Katiba.

Mahakama ya Rufaa, hata hivyo, ilimpa Ruto afueni ikiruhusu makato hayo kuendelea huku maamuzi yakisubiriwa mnamo Jumatano, Januari 10, 2024.

Rais Ruto ameapa kwamba mpango huo hautasisitishwa na yeyote, akisema nchi zilizotatua changamoto za makazi ziliuanza pindi zilipopata wazo hilo.

Alisema waliowasilisha kesi kortini kupinga mradi huo, ni mafisadi ambao hawataki kuona Kenya ikisonga mbele kimaendeleo.

Akiwa Eldoret, alirejelea kauli yake ya mambo matatu; mafisadi wachague kuacha wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, waende jela au atawepeleka mbinguni.