Makala

AKILIMALI: Stevia ilimponya kisukari, sasa ajitosa kwa kilimo chake

December 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

KWA miaka sita alikuwa akiugua ugonjwa wa kisukari uliomdhoofisha kiafya, lakini aliposhauriwa kutumia majani ya stevia kwenye chai na uji, ugonjwa huo ulitoweka kama umande.

Ni kupona huku ambako kulimchochea kuanza kukuza mmea wa stevia mnamo 2009 na kukumbatia kilimo hicho hadi sasa ambacho kimekuwa kitega uchumi kikuu maishani mwake.

“Nilikuwa mwele kutoka 2003 hadi 2008, nikiugua kisukari na hivyo singekunywa au kula vyakula vyenye sukari ya dukani. Maafisa kutoka shirika la Pure Circle walinishauri kutumia majani ya stevia ambayo yaliniponya,” anasema Joseph Osinyo Siango.

Mkazi huyu wa kijiji cha Gachuba, kaunti ya Nyamira anaeleza kuwa tangu apone ugonjwa huo, amekuwa akihamasisha jamii kupanda na kutumia majani ya stevia kukabiliana na kisukari huku pia wakipata hela kutokana na mauzo ya majani hayo.

“Nilianza kwa kukodisha robo ekari ya shamba baada ya kupewa mbegu na shirika la Pure Circle ambalo lilinihakikishia kununua zao langu kila linapokomaa,” anasema mkulima huyu wa miaka 59.

Kwa kila kilo moja ya stevia, shirika hilo humlipa Sh140, na kwa kila kila ekari anavuna kilo 200. Kando na mauzo ya mavuno ya stevia, yeye huuza miche kwa Sh100 kwa kila mche, biashara ambayo anasema inamtosha kujikimu kimaisha.

Ni mmea ambao husalia kwa kitangu kwa siku 30-40 ambapo mkulima anapaswa kuuhamisha kwa shamba lililolimwa vizuri.

Kwenye kitangu, unashauriwa kunyunyizia maji miche mara mbili kwa wiki, kulingana na hali ya hewa ukizingatia kuwa ili kupata sukari ya ubora wa aina yake, joto huhitajika.

“Baada ya kuhamisha, chimba mashimbo yenye kina cha futi moja mraba, tia mbolea na upande miche. Baada ya miezi mitatu, mimea yako itakuwa imekomaa na tayari kuvunwa,” anaeleza huku akiongeza kuwa mmea huu huweza kuvunwa kila baada ya miezi 3 maanake unapokata majani yake, majani hayo hukua upya.

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (KIRDI), mmea wa stevia una sukari mara 200 zaidi kuliko sukari ya dukani. Nusu gramu ya stevia inatoshana na gramu 12 za sukari ya kemikali.

Baadhi ya miche ya stevia ambayo Mzee Joseph Osinyo huuza ikiwa kwa katoni wakati wa warsha ya mafunzo ya Seeds of Gold mjini Kisii. Picha/ Faustine Ngila

Stevia ni mojawapo ya mitishamba ambayo hutumiwa kutengeneza baadhi ya dawa za mitishamba zisizo na kemikali wala madhara, na upanzi wake hauhitaji fatalaiza wala dawa za kemikali za kuua wadudu.

Mmea huu hupandwa katika maeneo yenye jua la kutosha, kwa mchanga usio na maji mengi, na mkulima huhitajika kuulinda dhidi ya magugu ili kuukinga dhidi ya magonjwa.

“Unapopanda kwa mara ya kwanza, hautahitaji kununua mbegu tena, ni mmea unaofanana na kitunguu saumu kwani unaweza kupanda upya vipande vyake,” anasema.

Kwa kila robo ekari ya shamba, mkulima hushauriwa kupanda miche kati ya 8,000 na 10,000 na kuacha upana wa sentimita 35 kutoka laini moja hadi nyingine na kiasi sawa kutoka mmea mmoja hadi mwingine.

“Baada ya kuvuna, PIWA Saccao hununua zao langu, wanaosha majani yake kisha wanatumia mashine ya kawi ya jua kuyakausha. Baadaye husagwa kuwa unga mweupe na kupakiwa kwenye karatasi tayari kwa mauzo kwenye maduka ya jumla,” anaeleza.

Utapata gramu 150 za stevia dukani kwa Sh995 lakini Bw Osinyo anasema ili kuepuka bei hii ghali, ni vyema mtu apande mmea wenyewe kwa shamba lake.

“Kutokana na uwezo wake kutibu magonjwa ya kisukari, moyo, tumbo, meno, nywele na kuupa mwili nguvu za kukabiliana na magonjwa, bei yake huwa juu sana na hivyo inawabidi watu kuukuza mmea wao wenyewe kupunguza gharama hii,” anasema.

Utafiti pia umeonyesha kuwa stevia ina uwezo wa kuwasaidia wenye uraibu wa kubugia pombe au kuvuta sigara kuondoa hamu hiyo na kukomesha kabisa mazoea.

Bidhaa hii inaweza kutiwa kwa vinywaji au vyakula na katika uokaji wa mikate na mahamri badala ya sukari ya dukani ambayo imeundwa kwa kemikali.

“Kwa maelezo zaidi kuhusu upanzi, ukuzaji na mbegu za stevia, unaweza kunipata kupitia nambari 0717497544 au 0787905558,” anawaambia wanaovutiwa na kilimo chake.