Habari za Kaunti

Wakazi wa Mukuyu walia eneo la biashara kugeuzwa dampo

January 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa mji wa Mukuyu katika Kaunti ya Murang’a wametoa malalamiko kuhusu rundo la taka ambazo zimeziba barabara muhimu.

Pia wachuuzi ambao hufanya biashara zao karibu na eneo hilo wamelalamika wakisema harufu mbaya na pia uvamizi wa wadudu hatari, unaweka wengi katika hatari ya kipindupindu.

Kwa pamoja sasa wanamtaka Gavana Irungu Kang’ata atoe sera maalum ya utupaji taka katika mtaa huo.

“Sisi ni kama tumeorodheshwa katika kiwango kimoja na nguruwe wapendao mazingira ya uchafu. Tumeteta lakini hatusikilizwi hadi tukaona tu tuvumilie huku tukimtumainia Mungu,” akasema mfanyabiashara mmoja, Bi Susan Njaraki.

Alisema haieleweki ni kwa nini utawala wa gavana Kang’ata uliamua kutenga sehemu ya barabara kama eneo la kutupa taka.

Aidha, taka hizo ziko mbele ya maduka na nyumba za wapangaji na kuzingirwa na wachuuzi ndani ya soko la Mukuyu ambalo huhudumia mamia ya wateja kwa siku.

Mkazi mwingine alisema kwamba “tukiwaambia kuhusu hatari ya hii taka huwa wanasema tunawapiga kisiasa”.

“Sisi tunatakiwa tunyamaze wakati wanatupiga kwa kutupa taka ovyo bila kujali hatari zake,” akasema mkazi huyo.

Bi Mary Muthoni ambaye ndiye Waziri wa Mazingira katika utawala wa Bw Kang’ata, alisema kwamba “nimepokea habari hizo na nitashughulika”.

Alisema kwamba juhudi za kulainisha mikakati ya utupaji na uzoaji wa taka katika mtaa huo zitaimarishwa.

[email protected]