Habari za Kaunti

Kamati ya usalama Kisii yalaumu wanasiasa kwa fujo eneo hilo

January 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

KAMATI ya usalama katika Kaunti ya Kisii sasa inawalaumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo hilo kwa ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila kuchao.

Kamati hiyo inayoongozwa na kamishina Tom Anjere, imedokeza kwamba baadhi ya wanasiasa, ambao haikuwataja, wamekuwa wakitumia nyadhifa zao vibaya na aghalabu wamekuwa wakihujumu utendakazi wa polisi kwa kuwatisha wanapojaribu kuchukua hatua za dharura kuzuia matukio yanayokiuka sheria.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya watu wanne kujeruhiwa kwa risasi katika eneobunge la Mugirango Kusini mnamo Jumatatu katika farakano lililohusisha Gavana wa Kisii Simba Arati na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro.

Gavana wa Kisii Simba Arati (kushoto) alidai gari la serikali ya Kaunti ya Kisii liliharibiwa na wahuni wa Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro mnamo Januari 8, 2023. PICHA | MAKTABA

Maisha ya raia wasiokuwa na hatia yalihatarishwa katika sehemu za Nyakembene pale watu wasiojulikana walivamia mkutano wa gavana Arati, uliokuwa wa kuwapa wanafunzi fomu za basari.

Gavana Arati alipokuwa akihutubu, watu wanaodaiwa kuwa wa Bw Osoro, walivamia na kufyatua risasi zilizoumiza watu wanne ambao walilazwa hospitalini.

Wengine wengi walipata majeraha madogo. Magari kadhaa yalipasuliwa vioo na wahuni walioteka shughuli hiyo.

Bw Osoro hata hivyo amekana madai hayo na kudokeza kuwa hakuhusika wala watu wake hawakupanga ufyatuaji wowote wa risasi.

Akilaani kitendo hicho cha kusikitisha cha Jumatatu, Bw Anjere alidokeza kuwa hawatamsaza mtu yeyote hata kama ana wadhfa upi.

Bw Anjere aliongeza kuwa tayari maafisa wa polisi walikuwa wameanzisha uchunguzi na kuahidi kuwa watafanya kila juhudi kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena.

“Tumekubaliana sote kwa pamoja kuwa hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika. Kama ni kiongozi ambaye alihusika pale, hatua zichukuliwe. Hatutaangalia cheo cha yeyote yule aliyehusika, awe ni MCA, awe ni mbunge, awe ni gavana, sheria lazima ifuatwe kwa makini,” kamishina Anjere alisema.

Aliwaomba wakazi wengine waliojeruhiwa kupiga ripoti katika vituo vyovyote vya polisi vilivyo karibu nao huku akiwaomba Wakenya wenye taarifa muhimu zitakazowasaidia kujitokeza.

“Nataka kutoa wito kwa viongozi wa gatuzi hili kuwa tunawaangalia. Tutawaheshimu ikiwa pia nyinyi mtaheshimu sheria. Hatuwezi kuendelea kuwekwa kwenye lindi la ukosefu wa usalama kuanzia Januari hadi Desemba. Tunayo majukumu mengine ya kutekeleza hapa silo hili tu. Wacha tuheshimu sheria na nyadhfa tulizo nazo,” Bw Anjere alifoka.

Mkuu huyo aliwataka maafisa wa polisi kufanya kazi yao ipasavyo na akawaambia wasitishwe na wanasiasa wowote.

Hakuna mtu aliyekamatwa kufikia sasa lakini Bw Anjere alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na tukio hilo la Nyakembene.