Bambika

DJ Fatxo asema 2024 ni mwaka wa kumweka Mungu mbele

January 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

BAADA ya kujipata pabaya mwaka 2023 alipohusishwa na kifo cha Jeff Mwathi, msanii tajika DJ Fatxo,27, sasa amekiri kwamba aliathirika, akiapa kutumia mwaka wa 2024 kumkimbilia Mungu.

“Waliniambia niende pale ambapo ninathaminiwa. Nikamrejelea Mungu aliyenipokea kwa mikono yote miwiili na akanipa amani na mwangaza. Haikuwa rahisi lakini nimevuka hadi kwa neema sasa,” akasema.

Aliweka msisitizo, akitumia lugha ya mtaa kwamba “ni Mungu tu manzee”.

Akipiga stori na safu hii, alisema kwamba akisimama katika kivukio cha mwaka wa 2014 aliwazia kuhusu masaibu yake ya awali lakini moyo ukajawa na furaha kwa kuwa aling’amua kwamba ujasiri ndio uliomhifadhi.

“Masaibu hayo niliyatumia kujielimisha kuhusu maisha na ushindi wangu nikagundua ulitokana na uvumilivu wangu na pia naMshukuru Mungu kwa kunihifadhi,” akaweka wazi.

DJ Fatxo ambaye ana upekee wake wa kucheza kila aina ya ala za muziki, aliondolewa lawama za mauti hayo ya Mwathi na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) licha ya kwamba jumuiya ya mitandao ya kijamii haikuridhika na imekuwa ikimrushia cheche za shaka ikimwandama kwa shutuma kali.

Hata hivyo, DJ Fatxo ambaye umaarufu wake ulitikisika baada ya mashabiki wengi kumhama na kumgeuza kuwa vibonde mitandaoni, amekuwa akijipamba upya huku baadhi ya marafiki waliokuwa wakikwepa kuonekana naye hadharani sasa wakimrejelea na kushirikiana kuchapa shoo pamoja.

Anasema kwamba hakuna siku hata moja hadi sasa amepumzika tangu msimu wa Krismasi uanze hadi kuingia Mwaka Mpya kwa kuwa amekuwa akiitiwa shoo zikifuatana katika maeneo mbalimbali ya burudani nchini.

“Wakati umejipata chini, uamuzi ulioko tu wa busara ni kujinyanyua na kuanza upya safari ya kupaa. Usiwe mwoga wa kujipamba upya kwa kuwa Mungu yuko nawe. Wengine wetu tuko hai kukupa motisha ya kukazana. Ukiniona mimi hapa, ukiyajua niliyopitia, jipe tumaini la maisha,” akasema.

Ufanisi wake mkuu ameutaja kuwa ule wa kuteuliwa katika tuzo za E360 katika viwango vya msanii wa Mugithi wa 2023 na pia ngoma ya Mugithi mwaka 2023 yake ya Mwomboko ikiteuliwa “na ninakuomba unipigie kura”.

Anakuelekeza hadi kwa tovuti ya e360awards.com ukapigie kura wimbo ‘Mwomboko’ kupitia kodi 265007 na yeye kama msanii wa mwaka kupitia 265102.

Kama ishara ya kwamba ataibuka mshindi katika hali zote, anasema “si ukubwa wa jimba ambao hulipa ushindi katika makabiliano bali ni ukali wa vita vyenyewe”.

Mfuasi sugu wa klabu ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, DJ Fatxo ambaye jina lake kamili ni Lawrence Njuguna Wagura pia hununua na kuuza magari kwa faidha.

Aidha, huuza mavazi ya mitindo kando na kuwa balozi wa brandi na bidhaa za kampuni.

Anaapa kuwa “liwe liwalo nitarejea katika upeo wa kipaji changu na kisha nijijenge kwa mapana huku nikimweka Mungu mbele”.

[email protected]