UPORAJI: Mamilionea bila jasho
Na BENSON MATHEKA
Huku Vita dhidi ya ufisadi vikiendelea kupamba moto, taswira ya jinsi baadhi ya watu waliokuwa maskini walitumiwa kupora mali ya umma na wengine wakigeuka mamilionea kwa kuuza ‘hewa’ imeanza kujitokeza.
Uchunguzi katika sakata ya Sh61 bilioni katika Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) umefichua kwamba, mmoja wa washukiwa Fredrick Sagwe karani katika shirika hilo alivyojilimbikizia mali ya mamilioni ya pesa ikiwa ni pamoja na nyumba nane za kifahari katika mtaa wa Green Park mjini Athi River.
Kulingana na wapelelezi, thamani ya nyumba hizo ni zaidi ya Sh160 milioni. Bw Sagwe, anayepata mshahara wa Sh150,000, anaishi nyumba ya Sh40 milioni, anamiliki magari kadhaa ya kifahari na kampuni ya thamani ya Sh50 milioni na aliweza kutumia Sh25 milioni kuandaa harusi yake.
Wapelelezi wanaochunguza vita dhidi ya ufisadi walifichua jinsi washukiwa kadhaa wa kashfa ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) walivyopata utajiri wa haraka kwa kuuza hewa.
Katika sakata ya pili ya NYS, familia ya Ngirita kutoka Naivasha, ilidaiwa kupata zaidi ya Sh465 milioni katika muda wa mwaka mmoja na miezi kumi.
Wapelelezi waligundua kuwa familia hiyo ilitumia pesa hizo kununua mali ya mamilioni ya pesa katika maeneo tofauti nchini na magari ya kifahari. Mali hiyo ilizimwa na serikali huku kesi inayowakabili ikiendelea. Kulingana na agizo la mahakama, familia hiyo haiwezi kuuza mali iliyonunua kwa kutumia pesa za ufisadi.
Katika sakata ya kwanza, iligunduliwa kuwa John Kago aliyekuwa akifanya kazi kama dereva katika benki moja jijini, alimiliki mali ya thamani ya mamilioni jijini Nairobi, kampuni ya kukodisha magari yakiwemo ya kifahari ya Range Rover na Mercedes S350. Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu Hesabu wa Serikali, Bw Kago alipokea zaidi ya Sh346 milioni kutoka kwa Bi Josphine Kabura na mshukiwa mwingine wa sakata ya NYS 1 Ben Gethi.
Bw Kago aliambia wapelelezi kwamba, alipatiwa mkopo wa Sh60 milioni na Bi Kabura, msusi ambaye yadaiwa alilipwa zaidi ya Sh791 katika awamu tatu kutoka NYS.
Bi Kabura aliyefichua jinsi alivyokuwa akibeba pesa katika magunia alihusishwa na kampuni 20 zilizodaiwa kupokea pesa kutoka kwa NYS.
Bw Gethi ambaye mali yake ilizimwa na serikali na watu wa familia yake akiwemo mama yake, walipata mali haraka ikiwa ni pamoja na ploti ya thamani ya Sh45 milioni katika mtaa wa Muthaiga North jijini Nairobi, nyumba ya thamani ya Sh63 milioni katika mtaa wa Rossyln na ploti ya thamani ya Sh35 millioni mjini Thika. Mama na dada yake walisemekana kumiliki mkahawa mmoja jijini Nairobi uliokadiriwa kuwa wa thamani ya Sh16 milioni. Kulingana na ARA,wakati mmoja Bw Gethi alilipwa Sh80 milioni kupitia kampuni ya Horizon Ltd.