Miguna Miguna amrudisha Larry Madowo darasani
NA WANDERI KAMAU
JE, alama anayopata mwanafunzi katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) ni ishara ya mafanikio atakayopata maishani mwake?
Kwa baadhi ya watu, hiyo ndiyo imani yao, ijapokuwa wengine huwa hawayaamini hayo.
Kwa mwanahabari Larry Madowo, imani yake ni kuwa, alama anayopata mwanafunzi kwenye mtihani wa KCSE si dalili zozote kuhusu mkondo ambao maisha yake yatachukua.
Mnamo Jumanne, Bw Madowo, ambaye kwa sasa anafanya kazi katika kituo cha habari cha CNN nchini Amerika, aliwashauri wanafunzi ambao hawakufanya vyema kwenye mtihani huo “kutoogopa chochote”.
“Nilifeli KCSE, kulingana na viwango vilivyokuwa vimewekwa wakati huo. Hata hivyo, mwaka uliopita, nilisafiri mara 45 kwa ndege na kuzuru mataifa 27. Alama ya B- niliyopata kwenye mtihani huo ilikuwa ya chini sana, kiasi kwamba nilishinikizwa kurudia Kidato cha Nne. Usikubali mtu yeyote akudhalilishe kwa vyovyote vile,” akasema Bw Madowo, kwenye ushauri kwa wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mtihani huo.
Hata hivyo, ‘ushauri’ wa Bw Madowo ulikosolewa vikali na wakili mbishi Miguna Miguna, aliyesema kuwa mwanahabari huyo “anawapotosha wanafunzi hao”.
“Larry Madowo ni mtu wa kupiga kelele tu. Wazungu wanaokiendesha kituo cha habari cha CNN huwapendelea watu kama yeye. Anadhani kuwa kusafiri katika nchi mbalimbali duniani ni mafanikio makubwa. Hatutamruhusu kuwapotosha watoto wetu kwamba kusoma na kupita vizuri hakuna maana yoyote,” akasema Dkt Miguna, Jumatano, kwenye ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter).
Ikizingatiwa wote ni watu maarufu, wenye ushawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii, kuna wale walioonekana kumuunga mkono Bw Madowo, huku wengine wakimuunga Dkt Miguna.
Je, wewe unamuunga mkono nani?