Siasa

Kamwene: Makau Mutua amkinga Kalonzo dhidi ya makombora ya Karua

January 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MSEMAJI wa Sekretariati ya mrengo wa Azimio la Umoja, Profesa Makau Mutua, amemtetea vikali kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, dhidi ya shutuma ambazo amekuwa akielekezewa na viongozi wa vuguvugu la ‘Kamwene’.

Mnamo Jumatano, kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu hilo, alilaani vikali hatua ya Bw Musyoka kulitaja kuwa la kikabila na lisilo na mustakabali wowote wa kisiasa.

Bw Musyoka alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano aliyofanya Jumanne na kituo kimoja cha televisheni.

Hata hivyo, mnamo Ijumaa, Prof Mutua alimtetea vikali Bw Musyoka, akiwataja wale wanaomkosoa kiongozi huyo “kutokuwa na ushawishi wowote kisiasa”.

“Wale wanaomshambulia Kalonzo kwa kukosoa vuguvugu lao la kikabila ni watu wasio na umuhimu wowote wa kisiasa. Ukombozi wa Kenya hautatoka kwenye miungano ya kikabila, bali kupitia muungano mkubwa wa kitaifa,” akasema Prof Mutua, kupitia mtandao wa X.

Kando na Bi Karua, viongozi wengine wa kundi hilo ni Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya kati ya wengine wengi.

Vuguvugu hilo linawajumuisha viongozi wa kisiasa wa Azimio kutoka eneo la Mlima Kenya.

Kundi hilo linadaiwa kuwa na ‘baraka’ za Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kauli ya Prof Mutua haifai kuwashangaza wengi, kwani amekuwa miongoni mwa wakosoaji wakuu wa Bw Kioni.

Bw Kioni amekuwa akipinga Ripoti ya Kamati ya Mazungunzo ya Kitaifa (NADCO), akisema kuwa haukujumuisha masuala yaliyowasilishwa na Azimio.

Wadadisi pia wanataja hilo kama ishara za migawanyiko ya kisiasa inayoendelea kupanuka katika mrengo huo.