Makala

Ruto ahama Ikulu ya Nairobi baada ya kuambiwa na wataalam ‘iko hatarini kuporomoka’

January 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto hatakaa katika Ikulu ya Nairobi kwa miezi miwili ijayo sababu ya ukarabati wa jengo hilo lililotengenezwa na wakoloni zaidi ya karne moja iliyopita.

Inaripotiwa kuwa wasanifu mijengo walionya kuwa huenda ikulu iliyojengwa miaka 117 iliyopita ikaporomoka.

Yamkini Rais, ambaye hupokea wageni wengi wa ughaibuni, alipendekeza matengenezo yafanywe badala ya kuunda ikulu mpya itakayogharimu mlipaushuru zaidi ya Sh2 bilioni.

Hata hivyo, mazingira ya Ikulu yamebadilika baada ya kukitwa kwa jukwaa jipya la kirais lenye uwezo wa kubeba mahudhurio ya watu 1,000 na 1,500.

Kiongozi wa Nchi alishinikiza kujengwa kwa ukumbi huu ili kupunguza gharama ya ukodishaji wa hema na utunzaji wa bustani uliofanywa mara kwa mara wakati wa hafla za Ikulu.

Kulingana na bajeti ya ziada ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024, Ikulu ilitumia Sh700 milioni kwa ujenzi wa jukwaa hili.

Bajeti ya Ikulu iliongezwa maradufu kutoka Sh4.37 bilioni hadi Sh8.85 bilioni katika mwaka wa kwanza wa Rais Ruto ikilinganishwa na kiwango cha bajeti ya mwaka wa mwisho wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Tangu mwanzo wa mwaka mpya, Rais amekuwa nje ya jiji la Nairobi akizindua miradi ya maendeleo Kaunti za Nyandarua, Nakuru na Uasin Gishu.

Mnamo Jumanne January 8, 2024, Kiongozi wa Taifa alipokea matokeo ya Mitihani ya Kitaifa ya Sekondari (KCSE) 2023 katika ikulu ndogo ya Eldoret alipokuw katika ziara ya kikazi Kaunti ya Uasin Gishu.

Vile vile, alikutana na sehemu ya viongozi wa chama cha Jubilee katika ikulu ndogo ya Nakuru Alhamisi Januari 11, 2024.