Salasya akamatwa kwa kuzua sokomoko tena kwa kumshambulia diwani
NA SHABAN MAKOKHA
POLISI wamemkamata Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya kwa madai ya kumshambulia na kumjeruhi diwani wa wadi ya Isongo-Malaha Bw Peter Walunya.
Katika malalamishi yake aliyowasilishwa katika kituo cha polisi cha Shianda, Bw Walunya alidai kuwa mbunge huyo na walinzi wake walimshambulia na kumjeruhi vibaya katika hafla ya mazishi katika wadi yake.
Diwani huyo aliwaambia maafisa wa polisi kwamba Bw Salasya alimshambulia baada ya wao kutofautiana kuhusu suala la itifaki.
“Tulikuwa katika mazishi ya Jesmus Kodia katika kijiji cha Maraba. Na nilikuwa jukwaani kuzungumza baada ya kumaliza nikamwalika mbunge huyo. Hapo ndipo akageuka na kunishambulia akisaidiwa na walinzi wake,” Bw Walunya akasema.
Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Mumias Mashariki Doris Chemos alisema walipata ripoti kuhusu fujo katika mazishi na walipofika huko, wakapata habari kuwa Mbunge Bw Salasya alikuwa amemshambulia diwani.
“Tulifaulu kumwokoa diwani huyo–Bw Walunya–ambaye aliandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Shianda kuhusu kisa hicho. Tulirejesha utulivu katika mazishi hayo na tukamkamata mbunge huyo. Lakini aliachiliwa huru kwa dhamana ya polisi ya Sh50,000 na atashtakiwa kortini Jumanne,” akasema Bi Chemos.
Walinzi wa Bw Salasya pia wamepokonywa bunduki kwa kufyatua risasi hewani, hali iliyowafanya waombolezaji kutoroka.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa Bw Salasya atashtakiwa kwa makosa ya kushambulia na kujeruhi mtu na kusababisha fujo na hivyo kuvuruga amani.
Video inayosambazwa mitandaoni inamwonyesha mbunge huyo akishambulia mwanamume mmoja aliyesimama kando yake akitoa hotuba.
Mumias East MP Peter Salasya arrested for assaulting MCA Peter Walunya at a burial in Mumias. pic.twitter.com/99vznYWqjf
— NTV Kenya (@ntvkenya) January 13, 2024
Baada ya kutoa pole zake kwa familia ya mwendazake, Bw Salasya alimsihi mwanamume huyo aketi chini.
Mwanamume huyo alipokaidi agizo hilo, Bw Salasya alimrukia na kumcharaza makofi, hali iliyozuia tendabelua katika mazishi hayo.
Walinzi wa Bw Salasya waliingilia kati na kumdhibiti mwanamume huyo kabla ya kumwondoa kwenye jukwaa.
Hii sio mara ya kwanza kwa Bw Salasya kuhusika katika makabiliano hadharani.
Mnamo Mei 2023, Bw Salasya alilaumiwa alipokabiliana na madiwani waliomzuia kuhutubu wakati wa mazishi ya aliyekuwa diwani wa Kisa Mashariki Stephen Maloba.
Aliokolewa na wabunge wenzake wakiwemo Omboko Milemba (Emuhaya) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda ambao walituliza hali.
Waliwashutumu viongozi hao kwa kuonyesha mfano mbaya kupigana hadharani mazishini.
Mnamo Novemba 23, 2023, Bw Salasya aliponea chupuchupu alipovamiwa na kundi la vijana kwa kumkosoa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa wakati wa hafla ya kanisa katika eneo la Bukaya, Mumias Magharibi.
Kando na hayo, Bw Salasya anayehudumu muhula wa kwanza, anachunguzwa kuhusiana na madai kuwa alitisha hakimu wa kike baada ya kumwagiza kulipa deni la Sh500,000 analodaiwa na mfanyabiashara Robert Lutta.
Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamemshutumu Bw Salasya kutokana na mwenendo wake wa kupigana hadharani na wanasiasa wenzake na raia wa kawaida.
Tafsiri na maelezo zaidi: Charles Wasonga