Mtaalamu wa IT ashtakiwa kufichua siri za mteja aliyepoteza Sh2.2m
NA RICHARD MUNGUTI
MTAALAMU wa masuala ya kiteknolojia katika benki mojawapo nchini ameshtakiwa kufichua siri ya akaunti ya mteja aliyepoteza Sh2.2 milioni.
Bw Simon Sirere Seno, afisa wa masuala ya kiteknolojia katika benki ya Cooperative, alishtakiwa pamoja na Harrisson Mwaura Njoroge kwa wizi wa Sh2.2 milioni kutoka kwa akaunti ya Bi Nancy Nyambura Kihanya.
Mabw Seno, Njoroge na Barack Ochieng Aluoch ambaye hakufika kortini, walikabiliwa na shtaka la kushiriki uhalifu kwa kutembelea matawi mengi ya Benki ya Cooperative kuiba wakitumia ujanja wa teknolojia kimtandao.
Mabw Seno na Njoroge walikabiliwa na shtaka la kuiba Sh2.2 milioni kutoka kwa akaunti ya Bi Kihanya iliyoko tawi la Cooperative Kayole, Nairobi.
Wawili hao walioshtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe walikanusha mashtaka sita.
Katika shtaka la kuunda njama za kuibia benki na wizi wa Sh2.2 milioni, Mbw Seno na Njoroge walishtakiwa pamoja, lakini Bw Seno alishtakiwa peke yake kwa kuvuruga mitambo ya kompyuta ya benki hiyo ya Cooperative.
Bw Seno alikana mashtaka manne ya kuvuruga mitambo ya benki hiyo na kuchukua taarifa za akaunti ya Bi Kihanya na kuzipeana kwa Njoroge.
Kufuatia kufichuliwa kwa taarifa za akaunti hiyo Sh2,210,241.50 ziilibwa kutoka kwa akaunti ya Bi Kihanya.
Mahakama iliombwa iwaachilie wawili hao kwa dhamana lakini kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech, alipinga akisema kuwa kesi hiyo itaunganishwa na nyingine inayosikilizwa na hakimu mwandamizi Bi Martha Nanzushi.
Bw Shikwe aliamuru kesi dhidi ya Mabw Seno na Njoroge itajwe mbele ya Bi Nanzushi itengewe siku ya kusikilizwa na washtakiwa waombe dhamana.
Hakimu huyo alifahamishwa na wakili aliyewakilisha wawili hao kwamba walitiwa nguvuni mnamo Alhamisi punde tu baada ya kusikilizwa kwa kesi nyingine inayowakabili.
“Wawili hawa walikamatwa pindi walipokuwa wanaondoka katika mahakama inayosikiliza kesi nyingine dhidi yao. Walizuiliwa katika kituo cha polisi na kufikishwa kortini bila hata kurudi makwao,” wakili alifichua.
Pia wakili huyo aliambia mahakama kwamba hakujua ikiwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi nyingine.
Wawili hao walizuiliwa tena hadi watakapofikishwa mbele ya Bi Nanzushi kutoa mwelekeo wa kesi hiyo.