Mafuriko yatatiza shughuli za kawaida maeneo mengi nchini
NA WAANDISHI WETU
SHUGHULI za kawaida zimetatizika katika maeneo mengi nchini kufuatia mvua iliyonyesha kuanzia Ijumaa na kuendelea usiku kucha hadi Jumamosi.
Katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba katika eneo la South B, kaunti ndogo ya Starehe jijini Nairobi, athari hasi za mafuriko zimeshuhudiwa.
Wakazi wamesema mvua ambayo imenyesha maeneo ya Kibera na Ngong imesababisha maji ya mafuriko kuja kwa fujo ambapo yamevunja kingo za Mto Ngong. Sasa daraja la Kayaba/Hazina halipitiki.
Vile vile makumi ya wakazi wa Mukuru-Kayaba wamelazimika kuondoka kwa makazi yao kwa sababu maji yameingia kwa nyumba.
Waandishi wa Taifa Leo wamewaona wakihamia katika nyumba za jamaa, majirani, na marafiki zilizo katika maeneo ya juu kiasi na hata zile za juu ghorofani.
Aidha waya inayopitisha umeme wa kiwango cha 33KV inaonekana ikipita katikati mwa mto huo wa Ngong, hali inayoweza kuwa hatari zaidi kwa sababu hitilafu ya nguvu za umeme inaweza ikatokea. Waya hiyo iko kwa paipu ya chuma.
Naibu Kamishna wa eneo la John Kisang amewaambia wakazi wahamie maeneo salama yaliyotambuliwa.
“Kwa sasa ninawafahamisha maafisa wa Kenya Power kuhusu hatari ya waya ya umeme kwa mto, hasa wakati wa mafuriko,” amesema Bw Kisang.
Ng’ombe wawili wa maziwa, vifaa kutoka kwa vibanda, na vyombo vya nyumbani, ni miongoni tu mwa vitu vilivyosombwa na maji ya mafuriko.
Wenye magari na wenye pikipiki hawawezi kuvuka daraja la Kayaba/Hazina kufikia barabara ya Enterprise na kisha Mombasa Road. Wamelazimika kutumia njia mbadala.
Kwa kiasi kikubwa mafuriko katika Mto Ngong yanasababishwa na mirundiko ya taka zilizosukumwa mtoni humo kwa sababu ya shughuli za binadamu bila utaratibu na wanyakuzi waliojenga kando ya mto.
Hali ni hivyo katika Kaunti ya Kajiado. Familia nyingi katika kijiji cha Noonkopir nje kidogo ya mji wa Kitengela zililazimika kuhama Ijumaa usiku kufuatia mvua kubwa iliyosabbisha mafuriko.
Wengi huishi karibu na mto wa msimu unaopita kijijini. Nyumba zilizingirwa na maji ambayo yaliharibu mali zao, yakiwemo malazi.
Bw David Simiyu,27, ameambia Taifa Leo kwamba familia yake ililala nje na kuvumilia baridi kwa sababu nyumba yao ya kupangisha iliyotengenezwa kwa kuta za mabati, ilizingirwa na maji ya mafuriko.
“Tulisikia sauti kubwa na kisha muda mchache baadaye, nyumba yote ilikuwa imezungukwa na maji. Hali ilikuwa ni ya kusikitisha,” amesema Bw Simiyu.
Naye mkazi mwingine, Bw Odanga Asiya, amelaumu mfumo duni wa kupitisha majitaka ambapo yote yaliishia kwa kijito hicho cha msimu.
Habari za Sammy Kimatu na Stanley Ngotho