Wenye baa wataja sababu za kuajiri mabaunsa nyamaume
NA RICHARD MAOSI
WAMILIKI wa vilabu vya burudani na baa jijini Nairobi wameomba serikali kulegeza kamba ili kuwaruhusu mabaunsa wenye miraba minne warejee kazini kukabiliana na wateja wakorofi.
Imekuwa ni vuta nikuvute, baadhi ya walevi wakionyesha kiburi na ujeuri, kwa kile wanachokidai wanalindwa na mkono mrefu wa serikali.
“Hali ikiendelea kuwa ya mwenye nguvu mpishe, itatengeneza mazingira mabaya ya kufanyia biashara,” akasema mmiliki wa baa moja eneo la Odeon katikati mwa jiji la Nairobi ambaye alijitambulisha kwa jina Terry.
Kulingana na Terry, anasema hawezi kuvumilia kero ya wateja kwa sababu anapitia mambo mengi kama vile makato ya juu ya ushuru, kodi ya eneo la kufanyia biashara na pia anahitaji kuwalipa wahudumu wapatao 30 kila siku.
Hata hivyo anaungama kuwa baadhi ya mabaunsa wamekuwa wakichoma picha na badala ya kutumia uungwana, wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kupita kiasi.
Lakini hiyo haifuti ukweli kwamba wanahitajika kuimarisha utulivu na usalama katika maeneo ya burudani, akasisitiza.
Katika vilabu vingi eneo la Mlolongo katika Kaunti ya Machakos, wamiliki wametoa malalamiko sawa na wenzao wa Nairobi.
Walidai kwamba kwa kipindi cha wiki moja mfululizo, walevi wamepata makucha ya kudunisha wahudumu na wamiliki wenyewe.
Bw Pius Muindi ambaye ni meneja wa kilabu kimoja Mlolongo, anasema sasa inalazimu kuchukua hela kwanza kabla ya kuwahudumia wateja.
“Hali hii mpya ya utaratibu inaonyesha kwamba mabaunsa wenye miraba minne wamekuwa wa msaada sana,” akasema Bw Muindi.
Kulingana na Bw Muindi, kazi haziendelei kama zamani, wateja na wahudumu wakiishi maisha ya mwenye nguvu mpishe.
Serikali sasa imeweka hitaji la mabaunsa kupatiwa mafunzo kuzuia visa vya kushambulia watu wasio na hatia.
Nalo Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK), limewasilisha kesi dhidi ya mmiliki na mabaunsa wa Kettle House Bar and Grill jijini Nairobi, kudai fidia ya wanahabari waliojeruhiwa, wakati wa msako uliofanywa na Mamlaka ya Kitaifa Dhidi ya Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada).
Akizungumza mjini Nyandarua, Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK Bw David Omwoyo, alisema baraza hilo litashinikiza fidia kwa wanahabari waliopata majeraha ya kimwili na vifaa vyao kuharibiwa Januari 6, 2024.
“Wakati huu, tumeamua kupiga hatua zaidi. Tunaenda kortini kudai fidia ya uvamizi huo,” alisema Bw Omwoyo.
Akaongeza: “Kesi hiyo ya uhalifu ikiendelea, baraza linaamini kuwa fidia hiyo ni njia mojawapo ya kukomesha vitisho na majeraha kwa wanahabari. Pia itawajibisha watu wenye mazoea ya kuhujumu kazi za vyombo vya habari na kuingilia uhuru wake.”
Bw Omwoyo alionya wamiliki wa biashara wanaounga mashambulio kwa wanahabari wenye vibali wakiwa kazini, akisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Wakati huo huo, aliwashauri wanahabari kuwa waangalifu wakati wa kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama.