Jinsi usasa unavyotutoa ujuzi wa kuwakabili fisi wala watu
NA WANDERI KAMAU
WANAVIJIJI sasa wamekosoa taratibu zilizotolewa kwa Wakenya na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) kwa wakazi wa eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, kuhusu njia za kukabiliana na fisi wala watu.
Mnamo Jumatano, shirika hilo lilitoa mwongozo kwa Wakenya kuhusu taratibu wanazofaa kuzingatia kuwakabili fisi ambao wamekuwa wakiwaua na kuwala watu katika eneo la Juja.
Mojawapo ya taratibu hizo ni kuwa badala ya kutoroka, wanafaa kusimama na kujaribu kumzungumzia fisi, ili kumshtua na hatimaye kuwaondokea.
Kutokana na kuongezeka kwa vifo vya watu ambao wamekuwa wakishambuliwa na fisi, baadhi ya wanakijiji katika maeneo tofauti nchini wamedai kuwa wamelelewa pamoja na fisi, huku wakikosoa vikali taratibu zilizotolewa na shirika hilo.
Kulingana na Mzee Francis Mwaniki, ambaye ni mkazi wa eneo la Marmanet, Kaunti ya Laikipia, njia moja ya kumshtua fisi ni mtu kujifanya ameketi na kuanza kuenda upande aliko mnyama huyo.
“Kwa sasa nina umri wa miaka 79. Nimekaa karibu na Msitu wa Marmanet kwa zaidi ya miaka 50. Nimekuwa nikitangamana na wanyamapori kama fisi, ndovu, ngiri, simba, chui, nyati kati ya wengine. Kwa kawaida, ni vigumu kuwasikia watu waliolelewa karibu na maeneo ya misitu wakiliwa au kushambuliwa na wanyama hao, kwani wanafahamu njia za kuwakabili na hata kuwafukuza,” akasema Mzee Mwaniki, kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.
Kulingana naye, mojawapo ya mafunzo ambayo watoto wanaozaliwa katika maeneo hayo huwa wanapata ni mbinu za kujikinga dhidi ya kushambuliwa na wanyamapori.
Mzee Mwaniki anaongeza kuwa njia nyingine ya kuwakabili wanyamapori, hasa ndovu na nyati, ni kubeba mwenge wa moto, hasa nyakati za usiku.
“Mbinu hii imekuwa ikitumika na wakulima katika maeneo ya misitu kuwazuia ndovu kuvamia mashamba yao na kuharibu mazao. Wanyama hao huwa wanatoroka wanapoona moto,” akasema.
Vile vile, kwa wanyama kama fisi, chui na simba, watu wamekuwa wakitumia vinyago vinavyofanana na binadamu kuwafukuza.
“Unapofahamu kuwa njia unayoelekea ina wanyama hatari kama fisi, ni vizuri kubeba kinyago chenye muundo wa mwanadamu. Hata ikiwa wanyama hawa huwa na ushujaa mkubwa, wakati mwingine huwa wanaogopa watu wawili na ambao hawatoroki. Akitokea, weka kinyago hicho mbele yako na usitoroke. Muundo wa kinyago hicho uonyeshe kama mwanadamu aliyeshika silaha kama panga ama bunduki. Kwa hilo, bila shaka huwa wanatoroka,” akasema.
Hivyo, anashangaa kuhusu ikiwa wakazi wa eneo hilo huwa wanawapa wana wao mafunzo kuhusu jinsi wanavyofaa kuwakabili wanyamapori wanapokutana nao.
“Ni nadra kusikia kisa cha mtu aliyeshambuliwa na fisi katika eneo hili kutokana na mafunzo ambayo tumekuwa tukitoa kwa watoto wetu. Swali ninalojiuliza ni kuhusu ikiwa watu wanaoshambuliwa na wanyama hao katika eneo la Juja ni wenyeji au ni wageni kutoka maeneo mengine nchini,” akasema mzee huyo.
Wanakijiji wengi walisema kwamba kuna uwezekano mkubwa watu wanaoshambuliwa katika eneo hilo si wenyeji, bali ni watu kutoka maeneo mengine wanaoishi huko.