KAULI YA WALIBORA: Baadhi ya shule zinakosea kuharamisha matumizi ya Kiswahili
NA PROF KEN WALIBORA
GAZETI la Daily Nation la Desemba 4, 2018 limebeba habari ya tamko langu kuhusu marufuku dhidi ya kuzungumza Kiswahili shuleni Kenya.
Limetoa tamko hilo nikiwa ziarani Embu nilipoalikwa na Dkt Timothy Kinoti kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Embu kuhutubu.
Marafiki zangu wengine kama vile Enock Bitugi Matundura wamenitaarifu kwamba tamko langu limesikika pia katika runinga moja muhimu humu nchini.
Hilo la kupewa umaarufu kwa kauli yangu niliyoitoa katika unyonge wangu sikutarajia. Nilifikiria kwamba ziara yangu ya Embu ilikuwa ziara ndogo ya mtu mdogo katika chuo kikuu chenye ukubwa wa kutisha.
Nilikuwa nikifikiria kuhusu polisi wa trafiki walionihangaisha karibu na mji wa Embu kwa madai kwamba leseni yangu ya kuendesha gari ilikuwa imepitwa na wakati.
Ilikuwa leseni ya miaka mitatu na tarehe yake ya kuongezwa muda ilipita kwa siku chache. Sikuwa na habari. Lakini waliniruhusu kuenda chuoni nitoe hotuba yangu. Hata hivyo, niliamua kukata leseni upya mjini Embu ili kuondokana na bughudha.
Kama ni hatia kwa dereva kuendesha gari bila leseni au na leseni ambayo muda wake umepita hilo, linakubalika. Na hili la mwanafunzi Mkenya kuambiwa ni hatia kuzungumza Kiswahili ni dhambi, si hatia tu.
Ndiyo maana nilitamka nilivyotamka kwa wanahabari walionisakama Embu punde baada ya hotuba yangu iliyosikilizwa na hadhira kubwa sana ya jumuiya ya Chuo Kikuu cha Embu.
Sikumbuki kuwahi kuona rubaa kubwa namna ile ya wanahabari na kamera na kalamu zao kama nilivyowaona huko Embu kwa ajili yangu! Hata ninapokwenda kwetu kijijini ambako sina jina jingine ila “Mtoto wa Mwalimu!” mapokezi kamwe hayawi kama hayo ya Embu.
Basi hapo ndipo mwanahabari mmoja mkakamavu aliponiuliza kuhusu sheria ya baadhi ya shule nchini kuharamisha matumizi ya Kiswahili nje ya darasa la somo la lugha hii.
Hii kwa kweli ni tanzia. Kwa nini Kiswahili kiharamishwe ilhali ni somo la lazima katika mfumo wetu wa elimu?
Mbona kizungumzwe tu wakati wa somo la Kiswahili? Kiingereza kinatumika hata nje ya mawanda ya ufundishaji wa Kiingereza.
Walimu wa Historia, Hesabati, Kemia, Jiografia, Bayolojia, wote wanatumia Kiingereza. Kwenye gwaride viranja na walimu wa zamu na walimu wakuu wanatoa hotuba zao aghalabu kwa Kiingereza.
Wanafunzi wengine wanasemezana wao kwa wao kwa Kiingereza hicho hicho. Labda wengine wanapolala wanaota kwa Kiingereza.
Huku kukwezwa kwa Kiingereza kunachusha na kuchosha. Aidha kunaenda kinyume na katiba na mwelekeo wa maendeleo endelevu ya kanda na utandawazi.
Katiba inasema Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi ya Kenya. Mwafaka wa kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unakipa Kiswahili hadhi ya kuwa lugha ya mawasiliano mapana.
Hivi karibuni bunge la Afrika Mashariki limekipisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jumuiya. Kuna mantiki gani kuharamisha shuleni kama si ucharamu?