Kambi ya Jeshi ya Moi kuhamishiwa Kerio Valley kukabiliana na majangili
NA WANDERI KAMAU
RAIS William Ruto Jumapili, Januari 14, 2024 alitangaza kuhamishwa kwa kambi ya mafunzo ya Jeshi la Kenya (KDF) kutoka Eldoret hadi katika Bonde la Kerio, kama njia ya kukabili wizi wa mifugo ukanda wa kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Rais Ruto alisisitiza kuwa serikali yake imejitolea kukabiliana na wizi huo, kwani umehangaisha eneo hilo kwa zaidi ya miongo minne bila dalili za kupungua kwake kuonekana.
Juhudi za serikali zilizopita kukabili wizi huo zimekuwa zikigonga mwamba, kwa sababu hali hutulia tu kwa muda, kabla ya visa vya wizi kuanza kushuhudiwa tena.
“Hizi ni ishara na dalili za mtindo huu kukoma. Tutakabiliana na wizi wa mifugo katika eneo hili tukiamini kuwa watu wa Bonde la Kerio watakuwa na amani. Hilo ndilo lengo ambalo serikali yangu inalenga kutimiza.
Jeshi halitaondoka katika eneo hili hadi pale hali ya amani itarejea. Tunajenga kambi kubwa ya polisi hapa. Kambi ya Jeshi ya Moi itahamishiwa katika Bonde la Kerio,” akasema Rais Ruto, alipokuwa akihutubu katika mji wa Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Rais Ruto alisema kuwa ununuzi wa vifaa na silaha za kisasa utaliwezesha jeshi kufurusha majangili kutoka maficho yao katika bonde hilo.
“Vifaa hivyo vitawasili nchini wiki ijayo. Vitatusaidia kukabiliana na ukosefu wa usalama kikamilifu. Tutahakikisha kuwa tutaziunganisha jamii zote katika eneo la Kaskazini, ili kuzungumza kwa lugha moja ya umoja,” akasema.