Samatta asema Taifa Stars ya TZ iko tayari kuizima Morocco
Na MASHIRIKA
ABIDJAN, Cote d’Ivoire
MSHAMBULIAJI hodari, Mbwana Samatta wa Taifa Stars ya Tanzania, amesema timu hiyo imejiandaa vyema kukabiliana na Morocco mnamo Jumatano ugani Stade de San Pedro.
Mechi hiyo itaanza saa mbili usiku, saa za Afrika Mashariki.
Hii itakuwa mechi ya kwanza kwa timu hizo tangu fainali za Afcon zianze mwishoni mwa wiki.
Ni miezi 13 tangu Morocco iweke historia kama nchi ya kwanza ya kutoka Afrika kutinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar, lakini Samatta amesisitiza kwamba ubora wao hauwatishi hata kidogo.
Akizungmza Jumanne kuhusu mechi hiyo ya ‘Kundi F’ inayotarajiwa kushuhudiwa na mashabiki wengi, nahodha wa Morocco, Romain Saiss alikiri kwamba itabidi wawe katika kiwango kizuri ili wapate ushindi, huku akisisitiza kwamba matokeo ya mechi zilizopita dhidi ya timu zenye uzoefu mkubwa yamedhihirishwa tosha kwamba mashindano haya hayatabiriki.
“Baada ya kung’ara katika fainali za Kombe la Dunia na kutinga nusu-fainali, tunatamani kuvuma zaidi hata hapa, lakini lazima tuwe tayari kabisa kucheza kwa kiwango cha juu ili tufike mbali,” akasema Saiss.
Watakapokuwa wamecheza na Tanzania, Morocco ambao wako katika nafasi ya 13 katika viwango vya ubora wa Dunia, watacheza na DR Congo na Zambia akmaarufu kama ‘Chipolopolo Bullets’.
Lakini Saiss ambaye zamani alikuwa beki tegemeo wa klabu ya Wolves, amedai kwamba lazima wapigane vikali ili wapige hatua inayofaa.
Morocco ambao wana rekodi mbaya katika mashindano haya ya bara Afrika, hawajafika fainali tangu washindwe na Tunisia 2-1 mnamo 2004.
Kikosi hicho cha kocha Walid Regragui kilicho kileleni mwa orodha ya mataifa ya Afrika, ni miongoni mwa timu zisizofanya vizuri katika michuano ya Afcon baada ya hapo awali kushindwa kutinga hatua ya makundi, mbali na mara mbili kutolewa katika robo-fainali miaka ya karibuni.
Tanzania inaorodheshwa katika nafasi ya 31 barani Afrika na 121 katika ubora wa Dunia, lakini kikosi hicho cha kocha Adel Amrouche kinajivunia mastaa kadhaa wanoacheza soka ya kulipwa katika mataifa ya kigeni.
Nahodha, Samatta anayechezea PAOK ya nchini Uturuki, ni miongoni mwa wachezaji walio na ujuzi wa mechi kubwa baada ya hapo awali kuchezea Genk, Fenerbahce na Aston Villa ya EPL nchini Uingereza.
Kuwepo kwa wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya Tanzania ni jambo zuri kwa kikosi hiki.
Kikosi hiki kina idadi kubwa ya nyota wanaosakatia klabu za ng’ambo ikilinganishwa na Taifa Stars iliyoshiriki Afcon 2019 nchini Misri.
Amrouche ana jumla ya wachezaji 14 ikilinganishwa na tisa waliokuwa Misri ambao ni Hassan Ramadhan wa Nkana ya Zambia, Himid Mao (Petrojet, Misri) Thomas Ulimwengu (Is Saoura, Algeria).
Wengine walikuwa Abdi Yussuf (Blackpool, Uingereza), Simon Msuva (Difaa El Jadida, Morocco) Rashid Mwandawa (BDF, Botswana), Yahya Zayd (Ismaily, Misri), Samatta (Genk, Ubelgiji) na Farid Mussa aliyekuwa akichezea CD Tenerife ya Uhispania.
Uchambuzi na maelezo zaidi yametolewa na John Ashihundu